-->

Header Ads

WATOTO NI DHAHABU


Namshukuru Muweza, Mungu mwenye huruma
Aliye nipa kuweza, nimeamka salama
Ninaanza na kuwaza, yale yaliyo na  hekima
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza
                   
Si vyema kuwapuuza,watunzeni kwa adabu
Kadhalika kuwabeza,yafaa mjitanibu
Vitendo vya kuchukiza, msiwe navyo karibu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Yafaa kuwatuliza, bila kufanya ghadhabu
Mazuri mkiwaeleza, watakuwa wastarabu
Hata wakiteleza, rahisi kujinasibu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Watoto mkiwakuza, umea kama zabibu
Wakubwa muwe wa kwanza, nyenzo zenu kuzitibu
Wadogo wanachukiza,kuwalea  kubwa tabu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Wewe Mungu kakukuza, daraja umekasibu
Na mwana ukimtunza, atageuka dhahabu
Hatua zake zakwaza, zinataka mahesabu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Abadani ukiweza, wewe ni bingwa tabibu
Lakini  ukiwabeza, kwa jazilizo la gubu
Utajichonga jeneza, kujitia magadhabu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Mimi siwapi bughuza, mkafura maghadhabu
Ila ninawaeleza, mpate japo taibu
Sifa ya mwana kutunza, na  sio kuwasulubu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Mwana anakengeza, na mwingine wa ububu
Allahu Rabi Muweza, hugawa pasi na kubu
Hatunabudi kutunza, pasipo ona aibu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

Pale mnapo wafunza, bila kuleta aibu
Wakutoa istiza, ukapata na swawabu
Tena nina sisitiza, mtoto ni kama dhahabu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza

La mwisho la kumaliza, sikia Bwana Hatibu
Zingatia bi Eliza, jiepushe  izarabu
Usijekunishangaza, tapokwona babu babu
Watoto kama Dhahabu, itunze  itakutunza














No comments

Powered by Blogger.