Majaliwa apiga marufuku watumishi kuwekwa ndani
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku
kuwekwa ndani watumishi wa umma, wakiwemo wauguzi kwa tuhuma za
kitaaluma.
Pia, amewataka wauguzi kufanya kazi kwa
weledi, uaminifu na kufuata maadili ya taaluma kwa kuwa maisha ya
wagonjwa yako chini yao.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatano akifungua mkutano mkuu wa 45 wa mwaka wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.
“Naagiza
viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya
kitaaluma, mabaraza husika yashughulikie jambo hilo na ni marufuku
kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma,” amekaririwa Majaliwa
katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jumatano.
Awali, Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa sekta ya afya bila ya kufuata utaratibu jambo ambalo si sahihi.
Waziri
mkuu amesema katika sekta ya afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa
kati ya wanataaluma wa afya, Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo
mikakati iliyopangwa kwa ajili ya kuiboresha.
Waziri
mkuu amewaasa wauguzi kuhakikisha wanazingatia kiapo cha maadili ya kazi
yao, akisema Serikali haitamvumilia yeyote atakayebainika kwenda
kinyume.
“Nanyi wauguzi mna wajibu wa kutoa huduma kwa
wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa
kuhusu baadhi ya wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kuomba rushwa
na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa,” amesema.
Majaliwa
amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika
ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya kuinua uchumi na
kufikia wa kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora.
Amewaomba
waunge mkono kwa nguvu zao zote jitihada za Serikali za kuhakikisha
miundombinu na vifaa vyote havihujumiwi na watu wachache ili viwe msaada
na hasa kwa wajawazito wajifungue salama.
Akizungumzia
upungufu wa wauguzi nchini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali
itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo wauguzi na
wakunga na kuwapanga katika maeneo yenye upungufu zaidi.
No comments