Kinywaji kinachosadikiwa gongo chaua watu watano Kimara
Dar es Salaam. Watu watano wamefariki dunia baada ya kunywa kitu kinachosadikiwa kuwa gongo eneo la Kimara jijini hapa.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Daniel Nkungu amesema kwa nyakati
tofauti kuanzia jana Jumanne jioni hadi saa nane usiku wa kuamkia leo
Jumatano walipokea miili ya watu wanne waliofariki kutokana na kunywa
kitu kinachosemekana kuwa ni gongo kutoka Kimara.
“Saa
nane usiku aliletwa mwanamume aliyekuwa hai lakini katika hali mbaya na
alifariki wakati anaendelea kupata huduma, hivyo kufanya waliokufa kuwa
watano,” amesema.
Dk Nkungu amesema kati ya waliokufa
mwanamke ni mmoja na miili yao imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili
kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha tukio hilo akisema atatoa ufafanuzi.
Taarifa
za awali zilizopatikana eneo la tukio zimesema waliokufa wanasadikiwa
kuwa tisa katika eneo la Kimara Stop Over na kwamba wengine kadhaa
wamelazwa kwa matibabu Mwananyamala.
Mwenyekiti wa Mtaa
wa Stop Over, Magreth Mugyabuso amesema, “Watu hawa inadaiwa walinunua
gongo ya viwandani wakaichanganya na vitu vingine, nadhani katika
utengenezaji kuna mambo walikosea hivyo kusababisha madhara hayo,”
amesema Mugyabuso.
Amesema alipata taarifa za tukio hilo jana saa sita usiku baada ya kupigiwa simu na polisi.
Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Saranga, Dandus Kijo ameeleza kusikitishwa na vifo
vya watu hao. Amewaasa wananchi kuacha kunywa pombe ambazo hazijapimwa
ili kuokoa maisha yao.
“Naelekea hospitalini
Mwananyamala kuangalia wagonjwa walionusurika kwa kuwa nasikia wengine
wamekuwa vipofu,’’ amesema Kijo alipozungumza na gazeti hili saa nane
mchana.
Share this story
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments