Mauaji Pwani yaacha machungu
Rufiji/Kilwa. Baada ya mfululizo wa mauaji ya viongozi wa Serikali za vijiji, vitongoji na kata katika maeneo ya wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga, sasa yameacha machungu na simanzi mji wa Kilwa katika familia nyingi.
Kwa Mkuranga, Rufiji na Kibiti tayari watu 31 wameshauawa kuanzia Mei mwaka jana, wakiwamo viongozi 15. Kwa kujumlisha na Kilwa, vifo ni viongozi wapatao 20 wa Serikali za Mitaa.
Vifo hivyo vimekatisha ndoto ya familia na kuwaacha wajane katika wakati mgumu kisaikolojia na kimaisha, huku wakiachiwa watoto wengi kulea.
Wajane wameachwa na watoto wengi wa kulea na sasa wanajipanga kuanza maisha mapya ambayo hata hivyo, hawana mwanga yatawafikisha wapi.
Wajane wawili kati ya watano ambao bado wanaishi katika Kijiji cha Bungu baada waume zao kuuwawa kikatili, waliongea na Mwananchi.
“Maisha yangu kwa sasa ni magumu sana kutokana na kifo cha mume wangu,” anasema Mwajuma Mustafa ambaye ameikimbia nyumba aliyokuwa akiishi na mumewe.
Mumewe, Mohammed Thabiti aliyekuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyang’undu, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akirudi nyumbani.
Anasema vibarua anavyofanya havitoshi kukidhi mahitaji ya watoto sita na kwamba hali ya maisha inazidi kumuelemea.
Nyumbani kwa Alife Mtulia, kiongozi mwingine aliyeuawa kwa risasi, hali ilikuwa ya majonzi.
Mtulia, aliyekuwa Katibu wa CCM wa Kata ya Bungu na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, aliuawa Mei 13 kwa kupigwa risasi nane wakati akielekea kuoga.
Mjane wa marehemu Mtulia, Zena Kimbungwi amepatwa na tatizo la shinikizo la damu na alishindwa kabisa kuzungumza na mwandishi wetu.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Omari Mtulia anaunga mkono mama yake asizungumze kutoka na tatizo hilo. Omari anasema mama yake alipata tatizo hilo baada ya baba yao kuuawa.
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments