-->

Header Ads

KWANINI UKO HIVI KWA MWENZAKO?


WEWE na mwenzako ni kama mwili mmoja. Kwa sababu hiyo na nyingine nyingi ndiyo maana mbali na kuwa na mamlaka na mwili wako ila mwenzako pia ana jukumu hilo.
Unaweza kuona nguo fulani dukani na ukanunua ila kutokana na sababu atakazotoa unaweza usiivae. Na si kuwa unaacha kwa sababu unamuogopa, hapana. Ila kuna heshima na hisia flani baina yenu zinazofanya kuona kama ukikataa jambo hilo kwa mwenzako hautakuwa na furaha kamili ya kuvaaa nguo husika.

Maana furaha yako inategemea namna anavyokutazama na namna anavyokuchukulia. Ikiwa mwenzako ana mtazamo hasi juu yako na wewe unalijua hilo, itakuwa ngumu sana wewe kuwa katika hali ya amani na furaha.

Halikadhalika na kwa mwenzako, ikiwa na wewe una mtazamo hasi juu yake hata siku moja hawezi kuwa na furaha na amani katika nafsi yake.

Na ili raha na amani kamili ya mahusiano iweze kupatikana, inabidi kila mmoja amjue mwenzako vizuri. Ikiwa unamjua mwenzako vizuri mahusiano yako hayawezi kuwa na shida na mashaka mengi. Utajua ufanye nini ili awe vipi, utajua ukifanya nini atasema nini! Unajua ni kitu gani anapenda mwenzako?

Ikiwa kweli unahitaji utulivu na furaha ya kweli katika mahusiano yako, kumjua mwenzako ni suala muhimu sana. Katika kumjua na kumuelewa ndipo utaweza kujua vizuri namna ya kufanya mahusiano yako yawe unavyotaka wewe. Nini anapenda mwenzako?

Ikiwa hujui ni vitu gani anapenda mwenzako, basi unajiweka katika mazingira ya kumfanyia mambo ya kumkera na kumdhoofisha kihisia. Ni kwa vipi utaepukana na suala hili ikiwa hujui ni kwa vitu gani huwa anakuwa katika hali gani?

Mbali na kumfanya kuwa na furaha na amani, ila kumjua mwenzako pia itachangia kumfanya ajue ni kwa namna gani alivyo na umuhimu katika maisha yako.

Ugomvi mwingi unaotokea katika mahusiano mbali na sababu nyingine ila pia huchangiwa na watu kutojuliana vizuri na matokeo yake unakuta mtu anafanya mambo ambayo mwenzake hayapendi. Unafikiri kwanini watu huachana ilhali wakati mwingine huwa bado wanapendana?

Ni kwa sababu kila siku huumizwa na baadhi ya mambo na kuona kama anafukuzwa kwa mlango mwingine. Amani ya mpenzi wako inakutegemea sana wewe kama ilivyo wewe kwake.

Ila pia una jukumu la kurekebisha ama kuzamisha mapenzi yako ikiwa hautakuwa makini katika matendo na maneno yako. Na kimsingi umakini baina yenu unajengwa kutokana na kiwango cha uelewa kwa mwenzako.

Yafanye mahusiano yako kama pepo ya mapenzi kwa matendo yako. Chunguza vitu vyote anavyopenda mwenzako. Isiishie tu katika vyakula na mavazi, hata aina ya vitu anavyoshabikia. Kwa kufanya hivi unakuwa unamsogeza karibu zaidi katika dunia yako ya mapenzi na kumfanya aone kwake wewe ni kila kitu.

Wengi wanawaumiza wenzao si kwa sababu wanapenda kuwafanyia hivyo, hapana. Ila ni kwa kuwa hawajui ni vitu gani wenzao wanapenda.

Pia hapa inabidi uwe makini na mjanja kwa maana mapenzi ya vitu kwa mtu yanaenda yakitofautiana. Kama ulikuwa na Jack anapenda mtu mkimya usidhani hata Hasan anapenda mtu wa aina hiyo. Hapa inabidi uwe makini na mjanja kumsoma mwenzako na si kutaka kuishi kwa mazoea.

Ikiwa utafanikiwa kumsoma  kwa makini na kugundua aina ya vitu vyote anavyopenda, hata ukiacha kuvifanya vyote ila utakuwa umetengeneza kitu kitakacholeta amani  na furaha sana katika mahusiano yako.

JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,

No comments

Powered by Blogger.