KUWA NA MSIMAMO, KATAA UTUMWA KATIKA NAFSI YAKO BHANA!!
NILIWAHI kumwambia binti mmoja hivi: “ Kama kasema hakuhitaji na katika nafsi yake kuna nafasi ya mtu mwingine, achana naye.” Hakukubali. Akasema hapana.
Akasema anampenda sana na moyo wake unamuhitaji kupita kima cha kawaida. Na hivyo yuko tayari kutumia kila uwezo, kila mbinu na kila njia ili awe na huyo mwanamume kwa kuwa anampenda sana. Sikushangaa sana. Mapenzi ndivyo yalivyo.
Wakati mwingine mapenzi yakitamalaki katika moyo wako, hata hatari iliyo mbele yako huwezi kuiona. Ndivyo ilivyokuwa kwa huyu binti.
Maana mbali na muhusika kuonesha toka awali dalili za wazi na za dhati za kutomuhitaji ila hakukubali. Akaamua kupigania penzi lake kwa kila namna. Na baada ya miezi mitatu, akafanikiwa kuwa naye.
Ila baada ya miezi mitano mingine, akarudi tena kwangu na kusema ahitaji tena mahusiano na yule jamaa. Sikushangaa sana. Mahusiano ya namna hii nayajua vema kama kiganja changu.
Binti akasema mbali na kumpenda na kumjali kwa kila hali, jamaa hana anachothamini kwake. Amekuwa jeuri, mkali bila sababu na wakati mwingine hata kumdharau yeye na familia yake. Kwa tabia hiyo msichana wa watu akasema amenawa mikono.
Tangu siku ya kwanza niliyaona haya katika uhusiano aliouhitaji. Kama mtu kakwambia hakuhitaji na zaidi anakuhakikishia kuwa yupo anayemgusa katika moyo wake na kuusisimua mwili wake, haina haja ya kuwa naye. Mara zote nasema hakuna mapenzi ya upande mmoja yanayoweza kuleta maana. Hata kama una upendo kama Malaika, ila kama hakupendi basi hakuna mapenzi timilifu hapo.
Kuna raha katika uhusiano pale kila mmoja anapokuwa na hisia na mwenzake. Pale kila mmoja anapomuona mwenzake katika uzani halisi wa mapenzi na furaha. Katika namna hii hata kama akiwa na tabia mbaya kiasi gani ila kama anakupenda anaweza kubadilishika na mkaishi katika maisha ya amani na furaha. Tatizo ni moja hapa.
Wengi wanaamini mapenzi ni suala la kuoneana huruma au kulipana fadhila. Japo fulani anaambiwa kuwa hapendwi ila hakubali na matokeo yake anahitaji kupata huruma kutoka kwa muhusika. Hii ni hatari sana.
Kitaalamu ni vema ukawa nje ya mahusiano kuliko kuwa na mtu ambaye yuko nawe eti tu kwa sababu anakuonea huruma. Eti anakukubali kwa sababu akikukataa utakuwa mnyonge na rafiki zake watamuita katili. Hii ni zaidi ya hatari.
Hata kama kesho atakubali kuwa nawe. Ila hakutokuwa na amani na furaha baina yenu. Mapenzi ya huruma hayaleti furaha. Mapenzi ya hisia za dhati ndiyo huleta amani na raha katika maisha.
Japo unampenda sana. Japo uko radhi kufanya kila kitu kwa ajili yake, ila kama hana hisia za dhati na wewe jua hakufai.
Bila hisia juu yako, hawezi kuwa mwema kwako, hawezi kukusikiliza, hawezi kukujali wala kutambua thamani yako katika maisha. Mtu huyu wa kazi gani?
Unaweza kulazimisha kuwa na fulani. Kwa kutumia pesa au hata watu fulani anaweza kukubali kuwa wako ila jua badala ya kuingia katika mapenzi unakuwa unaingia katika jela ya mapenzi.
Hawezi kukuchukulia kwa kina kama mpenzi wake wa dhati. Hata kama mtalala kitanda kimoja na kujifunika shuka moja, hata kama mtatumiana sana meseji, kuna hadhi fulani utaikosa katika maisha yake kama hana hisia na wewe.
Usikubali kuwa na mtu ambaye hana hisia na wewe. Hata kama unampenda ila kama anasema au anaonesha kwa dhahiri kuwa hakuhitaji katika maisha yake, ni vyema ukakaa naye mbali.
Wapo waliolazimisha kama huyo dada hapo, ila matokeo yake badala ya kupata raha wanayostahili wameambulia maumivu na madhila ya kutisha. Wanawafanyia kila kitu kizuri kinachostahili, ila wenzao ni kama hawaoni. Wanapendwa na kujaliwa ila ni kama wanatukanwa kwa namna wasivyoonesha kufurahishwa na matendo ya wenzao.
Ni raha sana kuwa na mtu unayempenda katika maisha, ila katu raha hiyo haiwezi kutimia kama mwenzako hakupendi.
Usikubali kuishi katika mahusiano ya kulipana fadhila. Kuwa katika mahusiano halisi. Yale yanayoundwa kwa hisia na kubarikiwa na matendo yenu. Hapo mbali na yote, ila kunakuwa na furaha na raha stahili miongoni mwenu.
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments