TATIZO SI NAFASI YA MWISHO, ANAJUA ALIPOKOSA?
HAKUNA binadamu asiyewahi kukosea. Kukosea ni suala ambalo lipo tu! Kila binadamu bila kujali hadhi yake wala umri, hukosea, japo pia kuna kukosea kimakusudi ambapo kwa mtu mwenye kujali na kutambua thamani ya kitu au mtu huwa na uwezo wa kuepuka.
Kwa kuwa kuna kukosea na hakuna binadamu mwenye uwezo wa kuishi kimalaika, pia inabidi kila mmoja anayekosewa asamehewe na kupewa nafasi nyingine.
Hii nafasi nyingine kimsingi si maana yake inaonesha kuwa umezoea kukosewa au kuwa kosa ulilofanyiwa halikuwa kubwa, hapana. Nafasi hii huwa mahususi kumpa mtu aoneshe ni kwa namna gani kosa alilofanya hakulitarajia na anajutia.
Japo unaweza kumpa nafasi hii na kukatokea akakukosea tena, ila huwa hatutarajii kuwa atakukosea kwa kosa kama hili. Kwa mtu mwenye kutambua thamani yako na maana ya kuwa na wewe anaweza kuwa na uwezekano mkubwa sana wa kukosea kwa sababu yeye ni binaadamu ila ni kwa asilimia ndogo sana anaweza kukukosea kwa aina hii ya kosa.
Umeumizwa sana na mpenzi wako? Amekufanyia mambo ambayo hutarajii na kufanya upate maumivu makali sana katika nafsi yako? Japo unaumia ila bado unahisi kumpenda. Japo unamuona kama hafai ila unahisi umuhimu wake katika maisha yako. Si ndiyo? Ndugu yangu, kukosea kupo. Hakuna binaadamu asiyewahi kukosea.
Haya matabasamu pamoja na vicheko unavyosikia kila siku nyumbani kwetu haina maana tunaishi kimalaika. Tunakoseana na pengine huwa tunakoseana sana kuliko ulivyowahi kukosewa. Ila kama binaadamu wenye akili na wenye kutambua kuwa kukosea ni moja ya hulka za kibinaadamu huwa tunatulia chini, tunakanyana kwa namna inavyofaa na maisha yanaendelea.
Na kwa kuwa kila mmoja anamjali na kumuheshimu mwenzake, huwa tunasahau yote yaliyotokea na kufungua ukurasa mpya wa mahusiano yetu. Ila kabla hujamaua kusema “nimekusamehe mpenzi wangu”, anajua kama kweli alikukosea? Anafahamu thamani ya chozi na maumivu aliyokusababishia?
Japo ni uungwana kumpa mtu nafasi ya pili ila ni ujinga kumpa nafasi ya pili mtu asiyejali. anaona kukosea kwake haikuwa inshu kubwa. Anadhani kuwa kwa kuwa yamepita basi yaachwe yapite.
Japo hatupswi kuishi na kumbukumbu za maumivu yaliyopita ila si rahisi kuzitoa kumbukumbu hizi kama muhusika haoneshi kuwa anajutia na anaumia kwa kile alichosababisha katika maisha yako.
Katika mapenzi mkosefu anabidi kuwa mnyenyekevu maradufu. Anabidi kuwa tayari kuwa mpole na ‘mjinga’ kwa dakika zote anazoomba msamaha kwa muhusika. Hii angalau humfanya muhusika ahisi amani na kuona kuwa mbali na yote ila bado thamani yake kwa mwenzake ipo.
Ukiona umekosewa na mkosaji anaomba msamaha kwa kawaida sana, hapo inabidi ujiulize kama kweli anamaanisha. Kusababishiwa maumivu na bado muhusika kuona kama alichofanya si kitu ujue kuna walakini hapo.
Kama kweli anahitaji nafasi ya pili kwa dhati inabidi aoneshe hali hiyo katika matendo na kauli zake. Inabidi awe tayari kukusikiliza, kukulilia na kukuona mfalme, malkia katika dakika zote za msamaha. Kufanya hivi haimaanishi hutumwa. Kufanya hivi haina maana kuwa wewe mkosewaji ni mzuri sana au tajiri sana, hapana. Hii ni tiba katika akili ya mkosewa.
Anapaofanyiwa hivi huona kuna hali ya kuonekana wa maana na wathamani. Hapa hata akisema kuwa nimekusamehe basi msamaha huo hutoka moja kwa moja katika nafsi yake na huwa unamaanisha kauli.
Hata kama kuna nafasi ya pili katika makosa ila nafasi hii haimhusu mtu asiyejua ukubwa wa kosa lake na maumivu ya jeraha aliyokusababishia. Tunasamehe ila ni kwa wale wenye kuonesha kwa dhati kuhitaji msamaha na kuona mahali walipokosea. Ahsanteni.
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments