Korti kusikiliza maombi ya Ally Saleh wa CUF
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia
mbali pingamizi la awali dhidi ya maombi ya kuizuia kufanya kazi Bodi ya
Wadhamini wa CUF, kambi ya mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi na Jaji Wilfred Dyansobera aliyetupilia mbali hoja za pingamizi zilizotolewa na wajibu maombi wakipinga maombi yaliyofunguliwa na Mbunge wa Malindi(CUF), Zanzibar, Ally Saleh.
Kutokana
na uamuzi huo, Mahakama itaanza kusikiliza maombi ya mbunge huyo
anayeomba zuio dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CUF ambayo wajumbe wake
waliteuliwa na Profesa Lipumba.
Akizungumza na
waandishi wa habari mmoja wa mawakili wa CUF, Juma Nassoro kwa upande wa
katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif amesema Jaji Dyansobera
ameamuru usikilizwaji ufanyike kwa njia ya maandishi.
Nassoro
amesema muombaji ametakiwa kuwasilisha hoja zake Oktoba 19 na wajibu
maombi wametakiwa wawe wamezijibu ifikapo Oktoba 27.
Amesema
Jaji Dyansobera ameelekeza iwapo muombaji atakuwa na hoja za nyongeza
awe ameziwasilisha ifikapo Novemba 4 na shauri litatajwa Novemba 6.
Mbunge
Saleh alifungua maombi hayo kutokana na kesi ya msingi aliyoifungua
mahakamani hapo akipinga uhalali wa wajumbe wa bodi walioteuliwa na
Profesa Lipumba.
Anaiomba Mahakama itoe amri
ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakala wao na watu wote wanaofanya
kazi kwa maagizo yao kutokujihusisha kwa namna yoyote na masuala ya
chama hicho mpaka uamuzi wa shauri lake la msingi utakapotolewa.
Wajibu
maombi ni Ofisa Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi
(Rita), aliyewakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wengine ni Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Malebo na wajumbe wa bodi hiyo.
Share this story
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments