-->

Header Ads

TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE YAWA MKOMBOZI AFRIKA MASHARIKI.. HIVI NDIVYO ILIVYOJIPANGA KIKAMILIFU

Na.Agness Moshi-MAELEZO

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekua mkombozi kwa wagonjwa wa moyo Afrika Mashariki kufuatia kupungua kwa gharama za matibabu ukilinganisha na ilivyokua hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo jijini Dar es Salaam, Mbunge wa  jimbo la Dokolo nchini Uganda Bi.Cecilia Barbara alipotembelea taasisi hiyo ili kuona na kujifunza  jinsi Serikali ya Tanzania inavyotoa huduma za Afya kwa wananchi wake .

Bi.Cecilia  amesema  taasisi hii ni msaada mkubwa kwa Afrika Mashariki kwasababu itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wa moyo wanaopelekwa  nchini India au Afrika Kusini  kwa matibabu kama ilivyo awali baadala yake watatibiwa Tanzania au nchini kwao.

“Tunahitaji kubadilishana mawazo kama wana Afrika Mashariki, kwasababu kwa kuja hapa tumegundua tunavifaa na uwezo wa kupunguza gharama za matibabu ya moyo“ Alisema Bi.Cecilia.

Bi Cecilia amesema  kutokana na ubora huduma zinazotolewa na taasisi hii  tangu kuanzishwa kwake  serikali ya Uganda imekubali  kuja kutembelea Tanzania ili kujifunza na kuanzisha mradi kama huu.

“Hatukujua kama Tanzania kuna mradi mkubwa kama huu na unaofanya kazi nzuri lakini kwa kuja tumejua na tunategemea kuanzisha mradi kama huu japo itatuchukua muda kufikia hatua iliyofikiwa na Tanzania”aliongeza Bi.Cecilia .

Naye Afisa Mwandamizi Kitengo cha Utafiti wa Bunge la Uganda Mhe. Jonathan Enamu  amesema kuwa amejifunza mengi kwenye ziara hii na ameona ni jinsi gani gharama za matibabu zimepungua kwa wagonjwa wa moyo. “Nimejifunza mengi, ikiwemo jinsi ya kupunguza  gharama za matibabu na namna bima za afya zinavyoweza kutumika katika matibabu“ alisema Bw. Enamu.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi  amesema kuwa , wanatoa huduma kwa watu wote kuanzia daraja la chini  na watu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Uganda,comoro,Yemen na Kenya.

 Prof.Janabi amesema kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kutumia shilingi bilioni 1.65 badala ya shilingi bilioni 4.72 ambayo ni sawa na kupunguza takribani asilimia 65 ya gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo nchini kama wangewapeleka India kwa matibabu

Prof. Janabi alifafanua kuwa kwa mgonjwa mmoja wa maradhi ya moyo anatibiwa kwa shilingi milioni 35-40 tofauti na nchini India ambapo mgonjwa mmoja anatumia shilingi milioni 120.

Aidha Profesa Janabi ameishukuru Serikali kwa kuipa ushirikiano taasisi hiyo kwani kwa mwaka huu wa fedha Taasisi imepokea asilimia 100 ya bajeti itakayosaidia kuendesha shughuli zao kwa kiwango cha kuridhisha.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na  Mbunge wa ilala Mhe. Azzan Mussa Zungu (MB) amesema  kuwa wamewapeleka  wageni hao kwenye taasisi ya moyo ili waweze kujifunza na kuona ni jinsi gani Tanzania imefanikiwa kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wa moyo

“wameona namna sisi Tanzania tulivyopunguza gharama kutoka kuwapeleka watu 300 kwa mwaka nje kwa matibabu ya moyo mpaka sasa watu wanne tu, ambao tunawapeleka si kwa sababu hatuna uwezo bali ni kwa sababu ya vifaa havijakidhi “ alisema Mhe.Zungu.

Taasisi ya  Moyo Jakaya Kikwete ilianzishwa rasmi mwaka 2014 inashughulika na utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wa moyo, kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari,ufamasia na uuguzi. Pia taasisi hii inashirikiana na nchi nyingine duniani kwa kubadilishana maarifa,uzoefu na kufanya mafunzo mbalimbali.                     

No comments

Powered by Blogger.