Korea Kaskazini: Kutokuwa na umuhimu Marekani kuwapiga marufuku raia wake kuja kwetu
| Bendera za Marekani na Korea Kaskazini |
Shirika la ustawi wa kieneo la Wonsan Zone
Development Corporation la Korea Kaskazini limetangaza kuwa, marufuku
iliyotangazwa na Marekani ya kuwazuia raia wake kufanya safari nchini
humo, haitakuwa na taathira yoyote kwenye sekta ya utalii.
Wonsan limeongeza kuwa, Pyongyang
inaiona marufuku hiyo kama isiyokuwa na umuhimu wowote. Msemaji wa
shirika hilo Han Chol-Su ameitaja hatua hiyo ya Washington kuwa
iliyosukumwa na siasa na kuongeza kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya
Pyongyang havina taathira yoyote na kwamba Korea Kaskazini itaendelea
kuimarisha harakati zake za makombora na silaha za nyuklia.
Shirika la Wonsan Zone Development
Corporation ni moja ya mashirika makubwa yanayojishughulisha na sekta ya
utalii nchini Korea Kaskazini. Ijumaa iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje
ya Marekani ilitangaza rasmi hatua ya kuwapiga marufuku raia wake
kufanya safari kwenda Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa takwimu
zilizotolewa, karibu watalii 5000 kutoka nchi za Magharibi hufanya
safari kwenda Korea Kaskazini kila mwaka ambapo kati yao 1000 hutoka
Marekani. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaonya raia wake kufanya
safari kwenda nchi hiyo ya Asia kutokana na hatari ya kutiwa mbaroni na
serikali ya Pyongyang. Hii ni katika hali ambayo Pyongyang inasisitiza
kuwa, inawatia mbaroni majasusi tu na sio raia wa kawaida.
Katika hatua nyingine Oleg Burmistrov,
naibu wa timu ya mazungumzo ya nyuklia kutoka nchini Russia amefanya
mazungumzo na Sin Hong-chol, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea
Kaskazini juu ya njia za utatuzi wa mgogoro wa eneo la Korea. Katika
mazungumzo hayo, Hong-chol amesema kuwa ikiwa Marekani itaendeleza
siasa zake za uhasama na vitisho dhidi ya Pyongyang, basi Korea
Kaskazini haitorudi nyuma hata kidogo katika kujiimarisha kwa silaha za
nyuklia na makombora ya balestiki. Oleg Burmistrov
amesema kuwa ameshuhudia mkwamo mgumu wa kisiasa juu ya suala la
utatuzi wa mgogoro wa eneo la Korea. Burmistrov aliyewasili mjini
Pyongyang siku ya Jumamosi, aliondoka mjini hapo jana usiku.
PARS TODAY
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments