-->

Header Ads

WITO KWENU WATUNZI

Tukutaneni wajuzi, magwiji  wa mashairi
Mafundi na wanafunzi, Sara na bwana Bashiri
Tuje na zetu kurunzi, tukajenge tafakari
Washairi mwasemani, ni swala makanikia

Tutungeni zetu tenzi,  ushairi ukifana
Kama hayati Mdanzi, mtunzi mzuri sana
Maneno yafate ngazi, tupange yakipandana
Washairi mwasemani, ni swala makinikia

Sisi pia ni wahunzi, mafundi kupanga vina
Hatujadili upuzi, uchambuzi wetu kina
Tunajulikana wazi, ni mabingwa wa kunena
Washairi mwasemani, ni swala makinikia

Njooni na wakufunzi, tena nawaomba sana
Watatua matatizi, pasipo ya kubishana
Tusiwe na pumbuwazi, pumbazo kushangazana
Washairi mwasemani, ni swala makinikia


Tuzitumie karama, jario la maulana
Tuitulize mitima, tujenge hoja za maana
Tutaepuka zahama, tukiacha chekeshana
Washairi mwasemani, ni swala makinikia


Sote mpate raha, pendezo la subuhana
Yanini hizi karaha, na kuzidi kushindana
Tunalifanywa majuha, mkubwa afanywa mwana
Washairi mwasemani, ni swala makinikia

Nanyi watunzi wa nyimbo, ninyi mnanguvu sana
Kwa ufundi wa kiimbo, na tungo zasikikana
Tu unasue urimbo, tena pasipo hiyana
Washairi mwasemani, ni swala makinikia







No comments

Powered by Blogger.