YANGA YAPITISHA BAKULI, WANACHAMA WAOMBWA KUCHANGIA.
UONGOZI wa klabu ya Yanga ukishirikiana na Kampuni ya Selcom umeanzisha akaunti maalum kwa ajili ya wanachama na wapenzi wake kuchangia pesa kwa ajili ya masuala mbalimbali ya uwendashaji wa timu hiyo.
Katika siku za karibuni klabu hiyo imekumbwa na ukata mkubwa huku ikielezwa baadhi wachezaji wake waliwahi kugoma ili kushinikiza malipo ya malimbikizo ya mshahara ya miezi mitatu.
Hata hivyo katibu mkuu wa klabu hiyo Boniface Mkwasa amewaambia waandishi wa Habari kuwa kuanzishwa kwa akaunti hiyo haimaanishi kuwa wameshuka kiuchumi ila ni kuiweka timu mikononi mwa wanachama ili waichangie katika masuala ya kimaendeleo.
“Yanga ina idadi kubwa ya wanachama nchi nzima kwa hiyo kupitia mfumo huu kila mdau ataweza kuichangia timu katika maendeleo ya klabu,” alisema Mkwasa.
Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni ya Selcom Galus Runyeta alisema mfumo huo utakuwa rahisi ambapo wanachama hao watatuma pesa kupitia mitandao ya M-pesa, Tigopesa na Airtel Money kwa namba moja ambayo ni 150334.
“Tunawaomba wapenzi na mashabiki wa klabu ya Yanga kuichangia timu yao kwa maendeleo yao kupitia namba 150334 ili waendelee kupata furaha,” alisema Runyeta.
TANGAZA BIASHARA YAKO NASI HAPA 0715 500 101 AU 0682 479 395
No comments