NI BASHITE: MAWAZIRI SUALA LA VYETI BUNGENI
WAKATI bajeti za wizara ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Utumishi na Utawala Bora zikipitishwa na bunge kwa matumizi ya mwaka wa fedha 2017/18 mwishoni mwa wiki, hoja moja iliwapa wakati mgumu zaidi mawaziri wa wizara hizo - cheti cha Bashite.
bali na hoja hiyo, mawaziri wa Tamisemi na Utumishi walijikuta katika wakati mgumu pia kujibu hoja juu ya uhaba wa watumishi na ajira mpya, ubovu wa miundombinu katika sekta ya elimu, watumishi hewa na wakuu wa wilaya kuwanyanyasa wenyeviti wa vijiji na mitaa.
Hoja ya cheti cha Bashite ni tuhuma za vyeti feki zinazomkabili Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Mawaziri George Simbachawene wa Tamisemi na Angellah Kairuki wa Utumishi na Utawala bora walipata wakati mgumu kujibu hoja hizo zilizoulizwa na wabunge waliokuwa wanataka kupata majibu ya uhakika.
Bajeti za wizara hizo ambazo ndizo zinagusa maisha ya watanzania kwa kiasi kikubwa, zilijadiliwa na wabunge kwa siku tatu kuanzia Jumanne hadi Alhamisi.
CHETI CHA BASHITE
Baadhi ya wabunge walihoji kwa nini mawaziri hao wanasuasua kuchukua hatua dhidi ya watendaji wa Serikali wanaotuhumiwa kutumia vyeti feki vya elimu wakati uthibitisho uko wazi.
Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago alishangaa Simbachawene na Kairuki kushindwa kuchukua hatua dhidi ya ‘Bashite’ ambaye anatuhumiwa kutumia cheti feki.
“Cheti cha Bashite kwa nini mnakilinda? Kwa nini hamtaki kuchukua hatua? Suala moja linazungumzwa mwaka mzima... kwa nini mnapata kigugumizi nyie mawaziri?” Alihoji Bilago.
Hoja ya Bilago ilimfanya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumuuliza “Unaposema Bashite unamanisha nini, ndiyo nani?”
Mbunge Bilago alisema “Bashite ni cheti cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.”
Hata hivyo wakati wa majumuisho ya bajeti zao, Mawaziri hao hawakuweza kulitolea ufafanuzi suala hilo.
TANGAZA NASI HAPA KWA BEI POA..
No comments