BAADA YA MANARA SIMBA YACHINJWA TENA, POINT TATU ZA MEZANI ZARUDISHWA KAGERA.
KISICHO riziki hakiliki! ndiyo kauli pekee ambayo unaweza kutumia kufuatia timu ya Simba kupokwa pointi tatu ilizopewa baada kupeleka malalamiko kuhusu beki Mohamed Fakih wa Kagera Sugar kucheza mchezo dhidi yao akiwa na kadi tatu za njano mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba Aprili 2.
Maamuzi hayo yametolewa na Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kufuatia Kagera Sugar kuomba mrejeo wa kesi (Review) kutokana na Kamati ya masaa 72 kuipoka pointi tatu na kuipa Simba.
Akitoa majibu ya Kamati hiyo Katibu mkuu wa TFF Celestine Mwesigwa alisema kamati hiyo imebatilisha maamuzi ya kamati ya masaa 72 yaliyoipa Simba pointi tatu kutokana na mambo matatu yaliyojitokeza hivyo matokeo ya mchezo huo yamebaki kama yalivyokuwa.
Mwesigwa alisema “Jambo la kwanza malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa kwa wakati kwa mujibu wa kanuni ya 20(1) inayotaka malalamiko yoyote kuwasilishwa bodi ya ligi ndani ya masaa 72.
“Jambo la pili malalamiko hayakulipiwa ada kwa mujibu wa kanuni ya 20 (4) ambapo inasema malalamiko yoyote hayatasikilizwa kama hayatakuwa yamelipiwa ada kwa wakati”.
“Jambo la mwisho kikao cha kamati ya masaa 72 hakikuwa na uhalali kutokana na kuwahusisha watu ambao walikuwa hawahusiki,” alimaliza Mwesigwa.
Mwesigwa alisema Kamati imemuagiza katibu mkuu wa TFF kuwapeleka baadhi ya viongozi wa bodi ya ligi mbele ya kamati hiyo kutokana na kupindisha ukweli juu ya sakata hilo.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba Simba ililala kwa mabao 2-1 ambapo sasa itabakiwa na pointi 59 ikiwa kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi tatu dhidi ya Yanga.
No comments