-->

Header Ads

Raia wa China waliokufa wakati wa ujenzi wa TAZARA wakumbukwa

Raia wa China wanaoishi Tanzania wamewakumbuka wataalam wa ujenzi wa reli inayounganisha nchi ya Tanzania na Zambia (TAZARA) waliofariki na kuzikwa nchini wakati wa ujenzi huo.
Kumbukumbu hiyo imefanyika Jijini Dar es Salaam katika eneo la Gongo la Mboto ambapo wataalaam hao walizikwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo una umuhimu wa kipekee kwani ni sehemu ya ukombozi na itaendelea kudumu kwa manufaa ya uchumi wa nchi mbili zinazohusika. 
“Ujenzi wa reli hii ulipanda mbegu ya ushirikiano katika sekta nyingine za maendeleo ambapo hadi sasa tunashuhudia miradi mingi ikiwemo ya viwanda vilivyowekezwa na Serikali ya China pamoja na kukua kwa biashara kati yetu,” alisema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga alimpongeza Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuona umuhimu wa kuwa na reli itakayounganisha nchi ya Tanzania na Zambia na kuamua kuomba msaada kwa Serikali ya China.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke amefafanua kuwa kumbukumbu hiyo imefanyika ikiwa ni siku ya maadhimisho ya utamaduni wa raia wa China iitwayo ‘Qingming’ yaani siku ya usafi wa makaburi ambapo raia wa China wameamua kuwaenzi wataalam wao waliozikwa nchini Tanzania.
“Zaidi ya wataalam 50,000 ambao ni raia wa nchi ya China walishiriki katika ujenzi wa reli ya TAZARA ambapo kati yao 65 walifariki, hivyo kumbukumbu hii inafanyika kwa ajili ya kuwaenzi wote waliojitolea nguvu na akili zao katika ujenzi huu,”alisema Balozi Wang Ke.
Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1860 ilijengwa kwa miaka sita tangu mwaka 1970 hadi 1976.

No comments

Powered by Blogger.