Mwalimu Nyerere anavyoishi mitandaoni
Dar es Salaam. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
anaweza kuwa aliondoka duniani mwaka 1999, lakini miaka 18 baada ya kifo
chake anaendelea kuishi; hotuba zake zimejaa katika mitandao.
Mwalimu
Nyerere, ambaye aliliongoza Taifa la Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961
na baadaye kuliunganisha na Zanzibar mwaka 1964, alifariki akiwa
London, Uingereza ambako alikwenda kutibiwa.
Aliliongoza
Taifa la Tanzania kwa takriban miaka 24 chini ya siasa za chama kimoja,
lakini baada ya kung’atuka mwaka 1985 alikuwa mtetezi mkubwa wa
demokrasia na hasa suala la kuandika Katiba bora itakayowapa wananchi
haki na nguvu ya kudhibiti viongozi wao.
Msimamo huo
ndio umemfanya Mwalimu Nyerere aendelee kuishi katika dunia ya leo,
kiasi cha vijana ambao hawakuwahi kumuona akiwa hai sasa wanamjua
kutokana na video zake kusambazwa kila mara kunapotokea tukio ambalo
aliwahi kulizungumzia.
Video za hotuba zake kwenye
youtube zinapata watazamaji kuanzia 1,600 hadi takriban 450,000 na
nyingi zina urefu wa kati ya dakika 1:58 na dakika 17:51
Lakini zile zinazorushwa katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na WhatsApp ni za urefu wa chini ya dakika 1:30.
Katika
hotuba nyingi alizowahi kutoa sehemu tofauti, inayosambazwa sana ni ya
mikutano yake na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani jijini Dar
es Salaam, ikiwamo aliyozungumzia suala la Muungano na umuhimu wa
kuheshimu Katiba na sheria.
Alilazimika kuitisha
mkutano huo na waandishi wa habari baada ya kuibuka suala la Zanzibar
kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kinyume na Katiba.
Hotuba
nyingine ambayo vipande vyake vinasambazwa kila mara kwenye mitandao ya
kijamii ni ile aliyoitoa alipoongea na waandishi wa habari Hoteli ya
Kilimanjaro, alipozungumzia sifa za mtu anayefaa kuwa rais na Muungano.
Lakini suala la Katiba ndilo limevutia sana watumiaji wa mitandao ya kijamii.
“Katiba
haiwezi kupuuzwa. Akishachaguliwa mtu ataapishwa kuilinda Katiba ili
tuweze kumshtaki aliyeikiuka. Mtu yeyote ambaye hawezi kuilinda wala
kuisimamia Katiba baada ya kuchaguliwa, hatufai,” anasema katika moja ya
hotuba hizo.
“Nchi haiendeshwi kwa matamko wala kwa
akili za mtu, bali kwa Katiba itakayowapa wananchi haki ya kufahamu nini
kitatokea kesho kwa kuwa hiyo ni haki yao.”
Vipande
vya video vya nukuu hizo vimekuwa vikirushwa mara kwa mara kwenye
mitandao ya kijamii kila wakati suala la Katiba mpya linapoibuka.
Na
wakati wanasiasa wa upinzani walipoibuka na hoja ya kutaka waendeshe
maandamano nchi nzima kupinga kile wanachokiita udikteta katika
operesheni waliyoita Ukuta, watumiaji wa mitandao hiyo nao walikuwa na
nukuu ya Mwalimu Nyerere inayoeleza maana ya neno hilo.
“Udikteta
ni serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Na wao ndiyo
huwa sheria. Anayepinga watakayo, basi huonyeshwa cha mtemakuni,”
anasema Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba hizo.“Tuzungumze. Mambo ya
nchi yazungumzwe waziwazi katika vikao rasmi vilivyowekwa. Nchi yetu
inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na maamuzi makubwa ya nchi yanatokana
na vikao na bungeni walivyotaka janja janja ya kuyatoa, hizi ndizo
dalili za dictatorship. Lazima zikemewe pamoja na janja janja.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, watumiaji wa mitandao walikuwa na ujumbe kutoka kwa Mwalimu Nyerere.
Katika
video hiyo, Mwalimu Nyerere anazungumzia umuhimu wa chama kuzingatia
maoni ya wengi wakati wanapoteua mgombea urais wa CCM, akionya kuwa
wakipuuza mambo yanaweza kutowanyookea.
Video hiyo ilisambazwa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM.
Akizungumzia
hali hiyo ya kuendelea kuishi kwa Baba wa Taifa, mratibu wa tathimini
na ufuatiliaji wa Baraza la Maaskofu (TEC) Paul Chilewa alisema
inatokana na watu kuona mawazo yake hayafanyiwi kazi.
“Changamoto
iliyopo sasa ni kwamba watu wanasikiliza hotuba zake, lakini
hawazifanyii kazi. Wanabaki kuzisifia kwa maneno, tofauti na
inavyotakiwa,” alisema Chilewa.
“Tunapaswa kusifia
hotuba hizo kwa kuleta matokeo chanya. Tujiulize tumepotea wapi? Je
kweli nchi inajengwa kwa maendeleo ya wengi au inanufaisha wachache?”
alihoji.
Naye Profesa Malise Kaisi alisema Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo wa kuona mbele.
“Aliona
umuhimu wa kuwa na siasa ya ujamaa na kujitegemea akisisitiza maendeleo
kwa watu na si vitu. Lakini kwa sasa kumekuwa na tofauti kwani
maendeleo ya vitu ndiyo yanapewa kipaumbele,” alisema Profesa Kaisi.
Alisema
ujenzi wa madaraja ya ghorofa (flyovers) au viwanja vikubwa vya ndege
katika kila mkoa, hausaidii kama bado huduma muhimu kwa wananchi
zitakuwa zinasuasua.
Naye Sheikh Khamisi Mataka, ambaye
ni msemaji wa Mufti, alisema: “Kuzungumzia maendeleo ya watu ina
maanisha waweze kupata vitu muhimu, elimu bora , chakula na mavazi na
afya bora.” alisema .
“Ili uendelee mbele kwa hatua ni
vyema uijue jana yako ilikuwaje je ulijikwaa wapi, ili uweze
kuitengeneza leo yako uweze kuipata kesho yako nzuri, wapo wanaosikiliza
na kufanyia kazi.”
Nyongeza na Beatrice Moses
No comments