-->

Header Ads

Waliomwagiwa kemikali wapelekwa KCMC

Wafanyabiashara wanne wa madini waliomwagiwa kemikali machoni wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyoko mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kiafya.
Wafanyabiashara hao ni pamoja na Sabas Laiser, Lucas Soto, George Nyakiha, Moringe Mollel pamoja na mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wadogo mkoani hapa, Ngalama Mapera.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi, Julai 27 mganga mfawidhi  wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Dk Jackline Urio amesema kwamba waliwapokea majeruhi hao juzi na kisha kuwapatia huduma ya kwanza kwa kuwaosha macho.

Dk Urio amesema kwamba wamewahamishia majeruhi hao katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi baada ya kushauriana na madaktari bingwa wa macho kutokana na hospitali yao kutokuwa na daktari bingwa wa macho.
“Changamoto tuliyonayo hapa ni kutokuwa na daktari bingwa wa macho hivyo tumeamua kuwahamishia Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi,”amesema Dk Urio.

Hatahivyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo amesema kwamba jeshi hilo mkoani hapa limefanikiwa kuwashikilia watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo na kusema kwamba pindi uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Ametaja wanaoshikilia kuwa ni pamoja na Schola Mwanga, Magreth Mushi, Sued Mwanga pamoja na Dorice Mushi.

Mkumbo, amesema kwamba watuhumiwa hao wanashikiliwa kutokana na kuwapulizia kemikali hiyo machoni baada ya kutofautiana katika malipo ya biashara ya madini waliyoifanya hivi karibuni.

JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,

No comments

Powered by Blogger.