-->

Header Ads

Ndama akutwa na hatia, atakiwa kulipa Sh200 milioni


.


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kulipa faini ya Sh200 milioni mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng’ombe baada ya kulikubali na kutiwa hatiani katika shtaka la sita la   kutakatisha dola za Marekani 540,000.

Akitoa hukumu hiyo leo Ijumaa, Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa amesema endapo mshtakiwa huyo atashindwa kulipa kiasi hicho cha fedha atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Hukumu hiyo ya shtaka la sita la kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na kuyakubali maelezo yote yanayounda shtaka hilo la  kutakatisha fedha,  akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Msigwa aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa amekubali shtaka la sita la kutakatisha fedha na maelezo yanayounda shtaka hilo.

“Hatuna kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya Ndama ila ni rai ya upande wa mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu cha 13(a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha,” imesema hati ya hukumu.

Amesema pia mahakama ibebe dhana ya sheria hiyo ambayo lengo lake ni kuzuia makosa ambayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi na uzito wa kosa ambalo mshtakiwa amelifanya.


Ameiomba mahakama izingatie maombi yao kwa sababu mshtakiwa huyo hilo ndiyo kosa lake la kwanza, kitendo chake cha kukiri kosa kinaonyesha kusikitikia kosa alilolitenda na kwamba anayo familia ambayo inamtegemea ambao kwa kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekaa ndani imepata shida kwa kukosa huduma yake.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 13(a) cha sheria ya kutakatisha fedha ni rai yetu mahakama tukufu isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu amejutia kosa alilolitenda,” amesisitiza Kung’e. Hivyo Ndama amehukumiwa kulipa faini ya Sh 200 milioni ama akishindwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Juni 6, 2017 Ndama aliiomba mahakama akumbushwe shtaka, akakumbushwa na Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson na akalikubali shtaka hilo.

Akisomewa maelezo ya awali mahakamani hapo, Ndama alikubali maelezo ya awali aliyosomewa ikiwamo nyaraka  zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika kuingizwa fedha hizo,  hundi 18 zilizotumika kutolea fedha hizo, maelezo ya benki ‘bank statement’ na Swift massage.

Iwapo atakamilisha kulipa Sh200 milioni atakuwa huru kuendelea katika mashtaka matano mengine yanayomkabili mahakamani hapo ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.

Ndama  anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na atoe fedha taslimu  kiasi cha Dola za Marekani 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya Sh600 milioni mahakamani hapo na  mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.



JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,

No comments

Powered by Blogger.