-->

Header Ads

JINSI WAISLAMU WA TANZANIA WALIVYOADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA QUIDS NA KUILAANI ISRAEL

Waislamu nchini Tanzania na wapenda amani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki leo wameungana na wapigania haki duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wao na muqawama wa wananchi wa Palestina mbele ya maghasibu Wazayuni.


Akizungumza na waandishi wa habari katika maandamano hayo jijini Dar es Salaam, Sheikh Hemedi Jalala Mkuu wa Chuo  cha Kidini cha Imam Swadiq (as) cha Dar es Salaam Tanzania ameyataja maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kwamba, yana umuhimu katika kufikisha ujumbe wa amani na kupinga dhulma za utawala vamizi wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Sheikh Jalala mmoja wa wanaharakati wa Kiislamu nchini Tanzania amesema kuwa, Imam Khomeini   (MA) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani iwe ni siku ya kukumbuka vitu viwili. Kitu cha kwanza ni kuukumbuka msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu. Sheikh Hemedi Jalala  ameongeza kuwa, jambo la pili ni kwamba, Imam Khomeini alitaka siku hii iwe ni maalumu kwa ajili ya kuwakumbuka wanyonge wote na watu wote wanaodhulumiwa duniani wakiwemo wananchi wa Palestina.


Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds Dar es Salaam Tanzania
Sheikh Jalala ameashiria dhulma na ukandamizaji unaofanywa katika maeneo mbalimbali duniani na akasisitiza kuwa, dhulma dhidi ya Wapalestina ni kubwa kuliko dhulma yoyote inayoshuhudiwa katika maeneo mengine ulimwenguni.

Sheikh Jalala ambaye pia ni Imam Mkuu wa Msikiti wa al-Ghadir wa Kigogo Post jijini Dar es Salaam amewataka Waislamu wa Tanzania na Waislamu wa dunia kwa ujumla wasiusahau msikiti wao na wasisahahu kibla chao cha kwanza  yaani Masjidul Aqswa ambacho leo kiko hatarini kutokana na siasa za kivamizi za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ameutaka Umoja wa Mataifa kushughulikia kadhia ya Palestina ili Wapalestina nao waishi kwa amani kama wanavyoishi watu wa maeneo mengine duniani.
Powered by Blogger.