RWANDAMINA KUIBOMOA SIMBA. AWATAKA AJIBU NA MKUDE.
RIPOTI maalumu ya kocha wa Yanga, George Lwandamina, itakayokuwa na tathmini ya msimu uliopita na mipango ya msimu ujao, huenda ikawabomoa mahasimu wao Simba.
Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Salum Mkemi, ripoti hiyo itakayokabidhiwa na Lwandamina wiki ijayo itatoa jibu kama watawasajili wachezaji watatu muhimu wa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Ibrahimu Ajib, Jonas Mkude na Mohamed Ibrahim ‘MO’.
Ajib na Mkude wamekuwa wakihusishwa kwa muda mrefu juu ya mpango wa kujiunga na Yanga, baada ya kumalizika kwa mikataba yao na wanaruhusiwa kujiunga na klabu yoyote, huku MO akiwa ni mmoja wa wachezaji wanaotakiwa na Yanga, jambo linaloweza kuibomoa Simba kutokana na mchango wa nyota hao kwenye kikosi hicho msimu uliopita.
Akizungumza na BINGWA jana, Mkemi alisema wanaisubiri ripoti itakayoandaliwa na kocha huyo wa Zambia ili kuifanyia kazi.
“Ligi imemalizika Jumamosi iliyopita na Lwandamina hajakabidhi ripoti yake, hivyo ni mapema kusema tunamsajili nani na kumwacha nani, hilo ni jukumu la kocha ambalo ataandika kwenye ripoti yake atakayoiandaa na kuileta kwetu wiki ijayo. Akina Mkude na Ajib watasajiliwa kama watajumuishwa kwenye ripoti hiyo ya kocha,” alisema Mkemi.
Lakini taarifa za ndani ilizozipata BINGWA kutoka kwa mtu wa karibu na Lwandamina zinasema wachezaji hao watatu ndio wanamtoa roho kocha huyo akiwapigia hesabu ili kuwanasa na kuongeza nguvu katika kikosi chake cha msimu ujao.
Pamoja na hao wa Simba, lakini Yanga wamedaiwa kuwa kwenye mchakato wa kunasa saini za mshambuliaji wa Toto Africans, Waziri Junior, viungo wa Mbeya City, Raphael Daudi na Kenny Ally, Salim Hoza wa Mbao FC, Michael Gradiel (Azam) na mlinda mlango Africa Lyon, Youth Rostad.
Katika hatua nyingine, Lwandamina alisema kikosi chake kinahitaji mabadiliko makubwa ili kuendana na hadhi ya klabu hiyo kitaifa na kimataifa, hivyo atawakabidhi uongozi wa timu hiyo ripoti itakayoshiba kabla ya dirisha kubwa la usajili kufunguliwa.
Source Bingwa
No comments