-->

Header Ads

RIPOTI MAALUMU: Hiki ndicho kiini cha mauaji Pwani


Nadharia nyingi zimeibuka juu ya lengo la watu wanaofanya mfululizo wa mauaji katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Pwani, lakini uchunguzi wa gazeti la Mwananchi umebaini kuwa uonevu na dhuluma ya muda mrefu wanayofanyiwa wananchi na kuenea kwa kasi kwa mafundisho ya dini yenye msimamo mkali ndizo sababu kuu.

Ingawa mamlaka zimeendelea kusimamia kile kinachoonekana kuwa makubaliano ya kutozungumza ni kwa nini, na ni nani anayetekeleza mauaji hayo, uchunguzi wa gazeti hili pamoja na maelezo ya wananchi na viongozi wao yanatoa mwanga juu ya kiini na sababu za mauaji hayo.

Uonevu na dhuluma iliyokithiri

Ni wazi kuwa wengi wa wananchi katika wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Kilwa ambazo mauaji hutokea ni masikini, wenye elimu ya chini na wanaoendesha maisha yao kwa kuvuna maliasili nyingi zilizoko katika maeneo yao na kuziuza.

Biashara kubwa ambayo vijana wanajihusisha nayo ni uchomaji na uuzaji wa mkaa, uvunaji magogo kwa ajili ya mbao, uuzaji wa kuni na mazao mengine ya mashambani kama vile mpunga na mihogo, imeajiri vijana wengi katika maeneo hayo.

Kutokana na hali hiyo, mamlaka za mitaa katika maeneo hayo umeweka vizuizi vingi vya barabarani vinavyoendeshwa na mgambo wa vijiji, maofisa wa maliasili ambao wakati mwingine hushirikiana na polisi kukusanya tozo na kodi mbalimbali za mazao ya misitu.

Kwa miaka mingi sasa, wananchi wamekuwa wakilalamikia vizuizi hiyo kuwa kitovu cha dhuluma na uonevu mkubwa wanaofanyiwa wananchi na wasimamizi wa vizuizi ambao wamekuwa wakikadiria kodi za kukomoa, kutaifisha magunia ya mkaa na mbao na mali nyingine za wananchi.

“Sababu kubwa ya haya yote ni mageti ya maliasili. Maofisa wa maliasili wanashirikiana na polisi kuendesha dhuluma kubwa,” anasema mkazi mmoja wa Rufiji kwa niaba ya wenzake waliozungumza na Mwananchi.

“Unanunua kitanda kati ya Sh70, 000 na Sh80,000 ukifika getini unaambiwa ulipe hadi Sh150, 000. Unaweza kuacha mzigo kwenda kutafuta pesa, lakini siku ya pili ukija watakwambia mali zako hazipo zimepelekwa makao makuu ya mkoa, ukienda mkoani wanakwambia hawajapokea kitu kutoka Rufiji. Hapa manaake vimeshaliwa,” anaeleza mkazi huyo kwa uchungu.

Anaendelea: “Kiroba cha mkaa nanunua Sh3,000 hadi Sh4,000 lakini unapotaka kupita pale getini watataka utoe kati ya Sh6,000 na Sh7,000.

Mwananchi mwingine wa Rufiji anaunga mkono maelezo hayo na kudai kwamba wanachokifanya polisi hivi sasa katika kuwasaka wauaji “ni sawa na kuwasha moto na kuuota mwenyewe.”

“Mageti haya haya ndio wanatoa vibali vya kusafirisha mkaa kwa Sh25,000 kwa siku tano, lakini unapokamatwa na watu wa maliasili au mkoa wanavikana vibali na wanakwambia huyo aliyetoa hana mamlaka ya kutoa.

“Hivyo wanakukamata, wanachukua pikipiki yako na fedha na kukwambia ulipe kiasi fulani ili kugomboa mali zako. Kesho ukienda hukuti kitu,” anadai mkazi huyo wa Rufiji.

Anasema uonevu na dhuluma vimechokoza hasira za vijana wengi.

Mkazi huyo anayejiaminisha kuwa anachokisema kinawakilisha mawazo ya vijana wengi wa Rufiji na Kilwa anasema chuki dhidi ya viongozi wa Serikali za Mtaa zilianza kuongezeka baada ya wao kushindwa kabisa kukomesha maonevu na uporaji wa mali za wananchi kwenye vizuizi.

“Vijana wengi na hata wazee walipoenda kwa viongozi wa kijiji kutaka msaada viongozi wanaishia kutoa majibu ya kisiasa mwaka hadi mwaka.

“Vijana wengi huku kazi zao ndio mkaa, kuni na mbao au mihogo. Sasa ukizingatia kuwa wana mafunzo mbalimbali, wengine walipita mgambo, wengine JKT na hawana ajira nyingine, wako hapa kijijini na wanafanya biashara hizo, ni hatari sana watu hawa wakiungana,” anasema.

Alipoulizwa wanapata wapi silaha, anasema: “Kila mtu ana mbinu yake ukizingatia mipaka yetu iko wazi.

“Vijana wengi wameuza viwanja vya baba zao na kuanza biashara ya mkaa. Sasa mtu wa namna hii ukimdhulumu kwa muda mrefu tegemea lolote,” anasema.

Anakataa maelezo kwamba mauaji hayo yanahusiana na mafundisho ya misimamo mikali ya dini.

“Si suala la kidini. Ni manyanyaso tu. Leo unadhulumu watano, kesho kumi, hawa wakiji-organise unatarajia nini?” anauliza, na kuongeza kuwa ingawa dhehubu moja la kidini limeteka vijana wengi lakini halina uhusiano na mauaji.

“Jiulize mbona hawavamii maduka. Mimi ni mkazi wa huku na ninakwambia ni haya mageti,” anasema.

Ushahidi wa kuunga mkono

Kuuwawa kwa Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya pamoja na maofisa wawili wa maliasili waliokuwa wakikusanya ushuru wa mazao katika kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti ni tukio linalounga mkono maelezo ya wananchi kuwa vizuizi vimekuwa kitovu cha maonevu Rufiji na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani.

Kabla ya kuua kwa risasi, wauaji waliteka kituo cha kukusanya ushuru wa maliasili na baadaye kuruhusu wananchi waliokuwa eneo hilo kuchukua mali zilizokuwa zimehifadhiwa na magunia mengi ya mkaa.

Wauaji hao takribani sita walifika katika kizuizi hicho muda wa saa sita usiku na kuwaweka chini ya ulinzi watumishi waliokuwa zamu na kuwataka kukaa kimya, wakisema kuna kazi ndogo waliyotaka kuifanya na baada ya hiyo wangeenda zao.

Kazi waliyotaka kuifanya ni kuruhusu shehena ya mkaa uliokuwapo hapo uchukuliwe na kila mwananchi aliyehitaji na waliwatangazia baadhi ya watu waliokuwapo eneo hilo kuuchukua mkaa ili wapate kupunguza makali ya maisha.

Wananchi waliokuwapo walihamasishana kuanza kuchukua magunia ya mkaa.

Kabla ya kuondoka wauaji hao waliacha mabango yenye onyo kwamba wataendelea kuua viongozi na kwamba hawatakoma kufanya kazi yao hiyo kwa madai kuwa wanawatetea wananchi ambao wamesahauliwa kupatiwa huduma muhimu.

Walisema kuwa ardhi iemekuwa ikitolewa kwa wawekezaji badala ya wazawa na wananchi wa chini wakinyimwa kujinufaisha na mkaa.

Waliacha pia orodha ya majina ya viongozi wa Serikali za Mitaa ambao walidai watawashughulikia kwa kuwa wamekuwa wanoko kwa raia na pia wanawanyima haki watu wanaowaongoza.  

source ; Mwananchi


JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,

No comments

Powered by Blogger.