-->

Header Ads

MAMA FUTA MACHOZI






Mja wetu Maanani, akujazilize siha
Uimarike moyoni, upate nguvu fasaha
Jifute chozi usoni, itengeneze furaha
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Waanamaji wa kwale, hufa maji mazoea
Tangu enzi zetu zile, mwiba guu huchelea
Hawaijui misukule, dogo kubwa potezea
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu


Acha kulia we mama, mwanao ashapotea
Jilinde uwe salama, tumai utazoea
Anayejua karima,wapi tunaelekea
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Alikuaga usiku, mama naenda safari
Safari kuchimba buku, twaenda kwa gari zuri
Ukafungua sanduku, ukampa na rozari
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Safari ni ndefu hatua, kufika ni majaliwa
Hakuna anayejua, ni lipi amepangiwa
Ile Fumba kufumbua, mwana jina kabakiwa
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Mama jivike ukambaa, kifua kivumilie
Sio vema kupumbaa, yakupasa utulie
Jiondoe vitambaa, vyafanya ujililie
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Ahadi zao puuza, hazita kufuta chozi
Mwanao umemuuza, basi usivimbe fizi
Ulisema utakuza, sasa giza la ajizi
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Pole yako iko wapi, faida kwao majengo
Walia paka sa ngapi, waache wenye vitengo
Vizazi vipo vingapi, Ala kaweka mtego
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Kifo cha mwana kipenzi, faida yake ni jengo
Wanakupaka masizi, wanakupindisha shingo
Wanakuvisha irizi, wanakukata mgongo
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu

Mungu wetu mpendevu, hulipa baya kwa wema
Jivike ukakamavu, kuyaona haya mama
Uwe mti mkavu, usiye pelekwa mrama
Mama jifute machozi, mtu si mali kitu







No comments

Powered by Blogger.