-->

Header Ads

UMOJA WA MATAIFA WATAKA KUINGILIWA MGOGORO WA LIBYA HARAKA


Kufuatia kuendelea vurugu na machafuko nchini Libya na kuweko uwezekano wa kuibuka tena vita vya ndani katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo, Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imeitaka jamii ya kimataifa iingilie kati mgogoro wa nchi hiyo na kuhitimisha machafuko ya ndani.

Baada ya kushadidi machafuko na mapigano, Fayez al-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya ameutumia ujumbe Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kuzitaka zichukue hatua za dhati na za maana mkabala na mashambulio na mapigano huko Libya. 

Waziri Mkuu huyo amesisitiza juu ya uungaji mkono wake kwa hatua yoyote ile itakayopelekea kupatikana amani na uthabiti nchini Libya. 

Kushtadi mapigano kusini mwa Libya ambayo yalianza baada ya mashambulio ya siku kadhaa ya vikosi vya jeshi la taifa kwa uongozi wa kamanda Khalifa Belqasim Haftar dhidi ya kituo kimoja cha jeshi kusini mwa nchi hiyo, kwa sasa kumeitumbukiza tena nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika hali ya kukaribia kuingia katika vita vya ndani. 
Fayez al-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya amelaani vikali shambulio hilo na kuahidi kufanyika mashambulio mapya yenye lengo la kuvitimua vikosi vinavyofungamana na jeshi la taifa chini ya uongozi wa Khalifa Haftar.


Fayez al-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya
Kabla ya hapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alitahadharisha kuhusiana na hali na mazingira mabaya yanayoikabili nchi hiyo. 
Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya sambamba na kutahadharisha kuhusiana na kuibuka vita vya ndani kusini mwa nchi hiyo, ameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati kwa haraka na kuhitimisha hali mbaya ya mgogoro inayoikabili nchi yake. 

Hivi sasa hali ya Libya imeendelea kuwa mbaya siku baada ya siku. Kuongezeka mapigano katika maeneo ya kusini mwa Libya na hofu ya kuzuka vita vya ndani katika maeneo hayo kwa upande mmoja na  kutetereka hali ya usalama kutokana na uwezekano wa kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi hususan la Daesh kwa upande wa pili, ni masuala ambayo weledi wa mambo wanayataja kuwa ni matatizo makubwa yanayoikabili Libya kwa sasa.

Mazingira hayo yameifanya hali ya kibinadamu nchini Libya izidi kuwa mbaya kila siku iendayo kwa Mungu. Takwimu za karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, takribani raia milioni moja na laki tatu wa nchi hiyo wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu. 

Hata kama hadi sasa kumefanyika juhudi nyingi za kisiasa ili kuikwamua Libya na mgogoro iliyonasa ndani yake, lakini juhudi hizo hazijawa na matunda bighairi ya kutiwa saini hati ya makubaliano ya Skhirat, Morocco na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. 
Kwa hakika makubaliano hayo kivitendo hayajaweza kuyavutia makundi  ya kisiasa ndani ya nchi hiyo kwa lengo la kuboresha hali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Jenerali Khalifa Haftar

Miongoni mwa vizingiti vikuu katika njia ya kufikia makubaliano na utatuzi wa matatizo ya Libya ni uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na hatua ya nchi mbalimbali ya kutaka kupatiwa hisa maalumu huko Libya. 

Siku zote Libya kutokana na kuwa na utajiri wa mafuta na nafasi maalumu kijiografia imekuwa ikikodolewa macho na madola ya kigeni. 
Hivi sasa pia madola hayo yamekuwa yakiyaunga mkono kwa kificho na dhahiri makundi mbalimbali ya kisiasa kama vile kuyatumia silaha na zana za kivita na kwa msingi huo kuendelea kuchochea kuni moto wa fitina nchini humo. 
Madola hayo yanafanya hivyo ili kufikia malengo yao. Suala jingine ni chaguo la hujuma ya kijeshi. 
Baadhi ya madola hayo yanataka Libya ishambuliwe kijeshi kama njia eti ya kuhitimisha hali mbaya ya machafuko na mgogoro inaokabiliwa nao. 
Hata hivyo wajuzi wa mambo wanaamini kwamba, madola hayo yana malengo maalumu yanayoyafuatilia huko Libya. 
Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Libya na makundi mbalimbali ya kisiasa ya nchi hiyo daima yamekuwa yakisisitiza juu ya kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Libya pasina uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
Powered by Blogger.