-->

Header Ads

WAHAMIAJI HARAMU ZAIDI YA 200 WAFA MAJI BAHARI YA MEDITERRANEAN


Zaidi ya wahamiaji haramu 200 wanaaminika kuwa wamezama baharini baada ya mitumbwi miwili waliyokuwa wakisafiria kugunduliwa na boti ya uokozi katika pwani ya Libya.

Laura Lanuza, msemaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya Uhispania iitwayo Proactiva Open Arms amesema, boti yao ya Golfo Azzuro jana iliopoa maiti tano zilizokuwa zikielea karibu na mitumbwi hiyo yapata kilomita 30 kutoka pwani ya Libya.

Ameongeza kuwa kwa kawaida mitumbwi hiyo huwa inabeba watu 120 hadi 140 kila moja.

"Hatudhani kuna kingine cha kuweza kueleza zaidi ya kwamba mitumbwi hii ilikuwa imejaa watu", amefafanua Lanuza na kuongeza kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hawajawahi kuona mitumbwi ya aina hiyo inayotumiwa na wahajiri ila huwa imefurika watu.

Amesema, maiti zilizopatikana ni za waafrika wanaume wenye umri kati ya miaka 16 na 25, na kwamba inavyoonekana walizama saa 24 kabla ya maiti zao kupatikana katika maji ya kusini ya bandari ya Libya ya Sabrata.


Mitumbwi inayotumiwa na wahajiri kusafiria
Licha ya hali mbaya ya bahari katika msimu wa baridi, idadi ya wahajiri na wakimbizi wanaosafiri kutokea pwani ya Libya kwa kutumia boti zinazosimamiwa na wafanya magendo ya binadamu imeongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) wakimbizi wengi zaidi walifariki baada ya kuzama katika bahari ya Mediterania katika kipindi cha wiki tisa za mwanzo za mwaka huu kulinganisha na kipindi sawa na hicho katika mwaka uliopita wa 2016.

Kwa mujibu wa IOM, zaidi ya watu 6,000 wameokolewa mnamo siku chache zilizopita katika bahari hiyo wakitoka Libya kuelekea Italia. Wahamiaji 16,248 tayari wamewasili nchini Italia mwaka huu ikiwa ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na 13,825 waliowasili katika kipindi sawa na hicho mwaka uliopita

No comments

Powered by Blogger.