Tatizo la Fangasi Ukeni ‘Vaginal Mycosis’
TATIZO hili huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa na husababisha uwepo wa maambukizi ukeni kutokana na fangasi. Hapa tunazungumzia fangasi ukeni, yaani kwa ndani lakini inaweza pia kushambulia nje ya uke na ikaitwa Vulvo Vaginal Mycosis kwa kuwa nje ya uke kunaitwa Vulva. Hali ya muwasho nje ya uke kitaalamu inaitwa Vulvitis .
CHANZO CHA TATIZO
Chanzo kikuu cha fangasi ukeni ni aina ya uoto wa ukeni uitwao Candida ‘monilia’ Albicans, ni uoto ambao ni hatari kwa kuwa huwa unakuwa sugu. Uoto huu hutegemea mazingira ya sukari iliyopo ukeni ambayo huhamasisha Candida kuota na kuongeza kiwango cha sukari ya Glycogen ukeni. Kuongezeka kwa kiwango cha sukari ukeni pia huwatokea hata wagonjwa wa kisukari ambao nao husumbuliwa sana na tatizo hili liitwalo kitaalamu Diabetic Vulvo vaginitis.
Hali kama hii ya fangasi ukeni inapotokea, hukolezwa zaidi na matumizi ya dawa za antibayotiki, kwa hiyo unapotumia aina hizi za dawa zinachangia fangasi kukua kwa kasi kwani zinaenda kusumbua mazingira ya walinzi pale ndani ya uke na wakashindwa kulinda uke kwa kutengeneza tindikali ya Lactic Acid.
Wanawake wengi hupatwa na tatizo la fangasi sugu kutokana na kutofanyiwa uchunguzi unaostahili na kujikuta wanaambiwa wana tatizo la yutiai, hivyo huendelea kutumia dawa za antibayotiki.
Ugonjwa huu wa fangasi hauna uhusiano kabisa na yutiai na hata uchunguzi wake hutofautiana.Tatizo huathiri ngozi laini na nje ya uke, mwanamke mwenye uoto huu huwa na rangi ya bluu na kugandia uchafu mweupe kama maziwa ya mgando au tabaka au ukoko.
DALILI ZA UGONJWA Dalili za ugonjwa ni muwasho mkali ukeni unaoambatana na uchafu mzito mweupe. Muwasho humkosesha mwanamke raha na kushindwa kutulia, mwanamke mjamzito pia husumbuliwa na tatizo hili la muwasho ukeni na kutokwa na uchafu mzito. Hali hii huanza kujitokeza hasa kati ya mwezi wa tatu wa ujauzito hadi mimba inapofikisha miezi nane.
Hapa mwanamke hulalamika muwasho ukeni na kutokwa na uchafu mara kwa mara. Tatizo hili kwa mjamzito linaweza kuisha kabisa baada ya kutibiwa kwa umakini au mara tu baada ya kujifungua lakini akishapata tiba. Hali hii ya kutokwa na ute mzito ukeni ambao hauna muwasho mkali, wengine hujituliza muwasho huu kwa kunawa au kujisafisha kwa maji ya moto. Usafi wa kutotumia vyoo vya kukaa kwa watu wengi pia itasaidia kuepuka matatizo haya.
UCHUNGUZI Ili kuthibitisha tatizo hili ni vema uchunguzi wa kina ufanyike kitaalamu kwa kuwa siyo kila hali ya kutokewa na uchafu ukeni ni fangasi. Hata kama mwanamke ana fangasi ni vema pia kutafiti chanzo ili lisije kujirudia.
Kama tulivyozungumzia, hali hii siyo yutiai kwa hiyo usije ukawa unatumia tu dawa za antibayotiki bila kupona na ukawa unazidisha tatizo ukajikuta mwaka mzima unaumia na ugonjwa mmoja.
Ugonjwa huu wa fangasi unaambukiza kirahisi, hivyo hata mwenzi wako naye anaweza kulalamika muwasho kwenye uume mara tu baada ya kumaliza tendo. Vipimo mbalimbali huwa vinafanyika kwa madaktari wa akina mama kama vile vipimo maalum vya ukeni na kuchukua sampuli ya uchafu huo na kupimwa maabara. Vipimo vya damu na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa vitafanyika.
No comments