Skendo: Hivi Ndivyo Madenti Chuo Kikuu Wanavyojiuza kwa Vigogo
DAR ES SALAAM: Mambo hadharani! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia Kikosi Maalum cha Kufichua Maovu cha Global Publishers (OFM) kuingia mzigoni na kubaini namna ambavyo wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam wanavyouzwa kwa vigogo wenye fedha zao.
Awali, makachero wa OFM walitonywa kuwa madenti wengi wa vyuo mbalimbali nchini wamekuwa wakiingia kwenye biashara hiyo haramu kwa kuunganishwa na madalali ambao baadhi yao ni wanafunzi wenzao.
“Sijui jamii yetu inaelekea wapi sasa hivi jamani! Baadhi ya wanafunzi wa vyuo kikiwemo kile Chuo Kikuu Dar wanauzwa kwa staili ya aina yake, wanakuwadiwa na wanafunzi wenzao ambao ndiyo ‘maajenti’.
“Ukimtaka mwanafunzi unamwona ajenti, anakuunganisha lakini huyo ajenti si kwamba unamlipa, yeye anakula kupitia mwanafunzi husika anayemuunganisha,” kilidai chanzo chetu cha habari.
OFM WAWEKA KIKAO
Baada ya kupokea ubuyu huo, makachero wa OFM walikaa kikao kifupi cha dharura kujadili namna ya kuchunguza madai hayo ili kubaini ukweli na mwishoni waliazimia kupandikiza wanafunzi ambao watakuwa maajenti na kuona kama kweli wataingia kingi. Zoezi zima likawa chini ya makachero wa OFM wa kutosha ambao walikuwa wakipigana picha hatua kwa hatua.
OFM KAZINI
OFM wakiwa kwenye muonekano kama wa wanafunzi wa hapo chuo, walijitawanya katika viunga mbalimbali vya chuo hicho na kazi yao ikawa ni moja tu, kufanya ukuwadi kwa baadhi ya wanafunzi wa kike ndani ya chuo na kuwaahidi kuwaunganisha na vigogo mbalimbali wenye fedha za kutosha ambao nao ni OFM vilevile.
Baadhi ya wanafunzi waliingia kwenye kumi na nane, na kwa namna mambo yalivyokuwa OFM ilijiridhisha kuwa kuna baadhi ya wanachuo wanatumia mbinu hizo kufanya biashara ya kujiuza.
DENTI WA KWANZA
OFM: Mambo vipi mrembo?
DENTI: Poa tu.
OFM: Mimi naitwa James, wewe unaitwaga nani vile?
DENTI: (akataja jina lake).
OFM: Ewalaa!…sasa unajua nini? Kuna kigogo mmoja anafanya kazi bandarini, huyu jamaa ana pesa chafu, mara nyingi huwa ananituma kwako anataka mtoke naye kwa pesa yoyote… unasemaje?
DENTI: Mpigie niongee naye (OFM anapiga simu kwa OFM mwenzake na OFM anajifanya yeye ni kigogo wa bandarini, wanaongea na kukubaliana kuonana na denti huyo kisha simu inakatwa).
DENTI WA PILI
OFM: Mambo vipi kadada, naona uko peke yako unajisomea, unaonaje tukiungana pamoja kusoma?
DENTI: Si unajua tena mitihani imekaribia… karibu.
OFM: Yeah nishakaribia, af’wewe huwa wanakuitaga nani vile? Na upo mwaka wa ngapi hapa chuo?
DENT: Naitwa (anataja jina lake), niko mwaka wa kwanza nachukua ‘Education’
OFM: Unajua nini, kuna mshkaji mmoja ni meneja wa Saccos moja hapa mjini, yule jamaa anakutaka kweli, tena hata mara moja tu, unasemaje?
DENTI: Sasa hivi niko bize na mitihani labda nikimaliza mitihani freshi..lakini kwa nini asije mwenyewe kwangu hadi akuagize?
OFM: Yeye yuko bize ndiyo maana kanituma mimi, ila kwa kuwa umekubaliana na hilo na umesema hadi umalize mitihani nafikiri atakuwa na subira hadi hapo utakapomaliza, au unasemaje mrembo?
DENTI: Haina tatizo, nikimaliza mitihani kila kitu kitakuwa poa, ingawa ni vema nikamwona mapema yeye mwenyewe mhusika.
OFM mbali na hao, ilizungumza na warembo wengine chuoni hapo ambao walionesha kukubaliana na biashara hiyo lakini wakaomba wapewe muda kwani kilikuwa ni kipindi cha mitihani.
OFM YAMALIZA KAZI
Hao walikuwa ni baadhi tu ya madenti katika wengi walionaswa na makachero wa OFM wakiwa tayari kuingia kwenye biashara ya kuuzwa kwa vigogo.
NENO LA MHARIRI
Ni vema wanafunzi hao wachache wakaachana na vitendo hivyo vya kukubali kirahisi kukuwadiwa kwa vigogo kwani kuna madhara makubwa wanaweza kuyapata.
Kwanza kuathirika kimasomo (kufeli), pili kuathirika kiafya (Kuambukizwa magonjwa ya zinaa) lakini tatu huwezi kujua huyo unayeunganishwa naye ana nia njema na wewe au mbaya. Habari hii iwashitue madenti wanaojirahisi kwa wanaume wasiowajua kisa pesa na wabadilike!
No comments