-->

Header Ads

Sudan yawahukumu jela wanaharakati watatu wa haki za binadamu


Mahakama moja nchini Sudan imewahukumu wanaharakati watatu wa haki za binadamu kifungo cha mwaka mmoja jela kila mmoja baada ya kuwapata na hatia katika kesi iliyohusiana na ripoti za uwongo.

Wakili aliyekuwa akiwatetea wanaharakati hao alithibitisha jana kuwa jaji wa mahakama hiyo ya Sudan aliwapata na hatia ya kuchapisha taarifa za uwongo au kufanya ujasusi wanaharakati hao watatu wa haki za binadamu waliokuwa wakifanya kazi katika taasisi moja inayotoa mafunzo kuhusu masuala ya haki za binadamu.

Jaji wa mahakama ya Sudan aliwapata na hatia ya kuchapisha taarifa za uwongo wanaharakati wawili waliotajwa kwa majina ya Khalafalla al Afif na Midhat Hamdan huku Mustafa Adam akipatikana na hatia ya kufanya ujasusi.


Mbali na kuhukumiwa jela, wanaharakati hao kila moja alitozwa faini ya dola 7,460. Wakili anayewatetea wanaharakati hao wa haki za binadamu amesema anatazamia kukata rufaa. Al-Afif, Hamdan na Adam walitiwa mbaroni tarehe 23 Mei mwaka jana baada ya askari usalama wa Sudan kuivamia ofisi yao huko Khartoum mji mkuu wa nchi hiyo. Katika kamata hiyo, jumla ya wanaharakati wanane walitiwa mbaroni lakini baadaye watano wakaachiwa huru.

No comments

Powered by Blogger.