NYANG’AU
Mie ni mtu makini, muenda
pole wa mwendo
Sipendezwi na utani,
jumba langu ni upendo
Tendi zangu ni deni,
uzisome bila bando
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Linanyonya waziwazi,
macho ukilifumbia
Ukilifanya ajizi, na halitakuvungia
Linakula na jambazi,
chumbani wajifungia
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Nyang’au hana busara,
shauri ajikatalia
Huluka zake za mara, tu
wazo likimjia
Tena hana fikara,
robo ukimpimia
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Naliona lajihami, tena
vingi vingorimbo
Hata anyosha ulimi,
naupenda huo wimbo
Hadhira hina usemi, imechoshwa
na vikumbo
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Maji yanapochemka,
hayasahau baridi
Ujipimie na miaka , upunguze ukahidi
Chafua uliko toka,
utajuta pa kurudi
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Kwa wema na upole,
dhamana uliiomba
Popo ni ndege Yule,
sifaze umezilamba
Leo nyuma kesho
mbele, unaendelea kuyumba
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Urongo si njia ndefu,
siku yako itafika
Nafuu yake hafifu,
tegemea hilo gaka
Umekosa utukufu,
kivuli umeongoka
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Urongo hauna dogo,
yapime uyasemayo
Usidharau madogo,
wasikize wasemayo
Mmea hukua gogo,
padogo huanziayo
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Nyang’au embu geuka, usiogope
kuchekwa
Usisite kuamka,
kushika yetu matakwa
Tunakutambua fika, rangiyo uliyopakwa
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
Mola nipe ushupavu, hila
zao kuumbuwa
Wakizidisha maovu, nizidi
kuwasumbuwa
Kwa beti zangu kavu, na
viriba napasuwa
Umegeuka nyang’au,
wanakuitaga mbojo
No comments