Jeshi la Syria laitungua ndege ya kivita ya Israel, Israel yapatwa na wasi wasi mkubwa
Komandi kuu ya jeshi la Syria imetangaza leo kuwa kikosi cha anga cha jeshi la nchi hiyo kimetungua ndege ya kivita ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wakati ilipokuwa katika safari yake kuelekea mji wa Palmyra, magharibi mwa mji wa Homs kuwasaidia magaidi walioshindwa wa Daeish.
Taarifa iliyotolewa na komandi kuu ya jeshi la Syria sambamba na kutangaza habari hiyo imesisitiza kuwa, asubuhi ya Ijumaa ya leo ndege nne za kivita za utawala huo katili sanjari na kukiuka haki ya kujitawala anga ya Syria ziliingia anga ya nchi hiyo kwa kutokea upande wa ardhi ya Lebanon katika eneo la Bureij.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege hizo zilianza kushambulia kambi ya kijeshi katika mji wa Palmyra lakini kikosi cha anga cha jeshi la Syria kilikabiliana na ndege hizo na kuitungua mojawapo, huku zingine zikilazimika kutoweka baada ya kuzidiwa. Jeshi la Syria limeongeza kuwa, hujuma hiyo imefanyika kwa lengo la makusudi la kuwasaidia wanachama wa kundi la kigaidi na utakfiri la Daesh ambalo hadi sasa linaonekana kushindwa kila upande na jeshi la serikali halali ya Syria. Aidha imesema kuwa, baada ya magaidi wa genge la Daesh (ISIS) kushindwa na jeshi la Syria, utawala wa Kizayuni unafanya njama kila uchao kwa ajili ya kuwapa moyo katika vita vyao dhidi ya Syria. Wakati huo huo komandi kuu ya jeshi la Syria imesisitizia azma yake ya kukabiliana na uchokozi wowote wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndani ya ardhi ya nchi hiyo na kuionya Tel Aviv juu ya chokochoko zake hizo.
Katika hatua nyingine mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa utawala wa Kizayuni ameelezea wasi wasi wake mkubwa juu ya uwezo wa hali ya juu ulioonyeshwa na jeshi la Syria hii leo na kusema kuwa radiamali ya jeshi hilo hii leo ni yenye kutiliwa shaka. Amir naami ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya utawala huo mapema leo kufuatia kutunguliwa na jeshi la Syria ndege hiyo ya kivita ya Israel na kusema kuwa, radiamali ya jeshi la Syria inatia wasi wasi mkubwa.
No comments