UN: Licha ya kupatikana amani ya kiwango fulani Darfur, bado Sudan inakabiliwa na hali mbaya
Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ukisema kuwa, licha ya kufikiwa usalama wa kiwango fulani huko katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan, lakini bado kuna mapigano ya mara kwa mara nchini humo.
Hayo yamesemwa na Aristide Nononsi, mtaalamu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sudan ambaye wiki iliyopita alifanya safari nchini humo na kuongeza kuwa kwa mara nyingine eneo la Darfur ambalo kwa miaka mingi limekumbwa na mauaji na machafuko na kisha kushuhudia usalama wa muda mfupi, limeanza kukabiliwa na machafuko na mauaji ya kikabila.
Mtaalamu huyo wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza aina tisa za ukatili ambao umekuwa ukishuhudiwa katika kambi ya wakimbizi baina ya tarehe 27 Januari hadi tarehe 18 ya mwezi huu kama ambavyo pia amewataka viongozi wa serikali ya Sudan kuwaachilia huru wanaharakati wa upinzani ambao wanaendelea kushikiliwa bila kufunguliwa mashitaka katika jela za nchi hiyo.
Inafaa kuashiria kuwa, katika harakati za maandamano ya kupinga uamuzi wa serikali wa kupandisha bei ya mafuta, polisi ya Sudan imewatia nguvuni wanaharakati kadhaa wa upinzani tangu mwezi Disemba mwaka jana hadi sasa. Aidha Aristide Nononsi ameashiria ongezeko la vitendo vya wizi, ukiwemo wa kutumia silaha, mauaji, ubakazi, ukatili na mapigano ya kikabila na kuongeza kwamba ni mambo ambayo yameshtadi jimboni humo. Kwa mujibu wa afisa huyo wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu, migogoro ya kikabila ni tatizo kuu jimboni Darfur.
Afisa huyo pia amesema kuwa hadi sasa machafuko nchini Sudan yamesababisha kwa akali watu laki tatu kuuawa na wengine milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi
No comments