Hatimaye jeshi la Iraq lakomboa uwanja wa ndege wa Mosul, Daesh wakaribia kushindwa rasmi
Sambamba na kuanza hatua ya pili ya operesheni za kuyasafisha maeneo ya magharibi mwa Mosul, kaskazini mwa Iraq, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kudhibiti uwanja wa ndege wa mji huo ambao ulikuwa ngome kuu ya magaidi wakufurishaji wa Daesh (ISIS.)
Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Iraq imesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limetumia mashambulizi mapana ya kila upande katika kuukomboa uwanja huo wa ndege wa al-Ghazlani kusini magharibi mwa mji wa Mosul. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa polisi wa federali na kikosi cha radiamali ya haraka ya jeshi la Iraq wamefanikiwa kusonga mbele na kuwaswaga wanachama wa genge hilo la kigaidi kutoka uwanjani hapo.
Inaelezwa kuwa, awali magaidi hao walitumia zana mbalimbali za kijeshi ikiwemo ndege zisizokuwa na rubani kwa lengo la kulizuia kusonga mbele jeshi la Iraq, juhudi ambazo hata hivyo zimeishia kufeli. Habari zaidi zinaarifu kwamba mamia ya wakazi wa maeneo ya magharibi mwa Mosul wameziacha nyumba zao na kwenda maeneo mengine kwa ajili ya usalama.
No comments