Hakimu awataka Kitilya, Wenzake kuwa na subira

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake kuwa na imani pamoja na subira dhidi ya upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili kwa kuwa unakaribia kufika mwisho.
Hayo yamesemwa leo Jumatano na Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Kabla
ya Hakimu Mkeha kusema hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi
Mutalemwa alieleza kuwa mara ya mwisho waliomba siku 14 ili waweze
kuelezea hali ya upelelezi ulipofikia lakini wameshindwa hivyo wakaomba
kuongezewa muda ili tarehe ijayo waweze kueleza.
Alieleza kuwa wanafanya jitihada kuona upelelezi unakamilika na akaomba tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Baada
ya Kishenyi kueleza hayo, wakili wa utetezi, Masumbuko Lamwai alidai
kuwa kesi ilifikishwa mahakamani hapo Aprili Mosi, 2016, hivyo ni karibu
mwaka mmoja na nusu sasa, mashtaka yanayowakabili wateja wake
yanahusisha nyaraka ambazo wanazo na kwamba hakuna uchunguzi nje ya
nyaraka.

"Kwa mtu anayekaa gerezani kwa mwaka mmoja na nusu, kuambiwa upelelezi bado haujakamilika inaleta mshangao.
"Hii
kesi imekuwa kama ya kukomoana komoana hivi, mheshimiwa wateja wetu ni
watu wazima wanashughuli zao na nyingine zimefilisika kwa kukosa
usimamizi," ameeleza Wakili Lamwai mahakamani hapo.
"Tunajua mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi hii lakini upande wa mashtaka wanatumia vibaya taratibu za kimahakama."
Baada
ya kutolewa kwa maelezo ya pande hizo zote mbili, Hakimu Mkeha
amewaambia washtakiwa kuwa upelelezi unaofanywa unakaribia mwisho
akaomba wawe na imani, kwa kuwa amejiridhisha yeye mwenyewe kwa macho
yake kuwa upelelezi unakaribia kufika mwisho.
Kesi hiyo
imeahirishwa hadi Oktoba 5, 2017. Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na
kesi hiyo ni maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula
njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola
milioni 6 za Marekani.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo
kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola
za Marekani 550 milioni kwa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya
Standard Uingereza.
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,