-->

Header Ads

KIBITI JASHO LA DAMU


Sisi wana Tanzania, Baba na akina mama
Kwanini twajililia, twatakiwa kusimama
Wao wanafikiria, hadha haiachi koma
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Tusiwe mapunguani, tusiojua alama
Inayotakiwa kani, kuulilia uzima
Kupigana mapigani, wima hata kuchutama
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Hili jambo si utani, legelege kusimama
Si utani wa jirani,na mzaliwa na mama
Tulinde yetu amani, watu tukae salama
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Tuipeleke amani,kwa akili na hekima
Busara ziwe vichwani,tupambane tukipima
Jambo si la vitabuni,tulitafakari vema
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Wana  hawatoki ndani,Wawahofia khasima
Kama tulivyo amini,tangu zamani za zama
Hii nchi ya amani , yafatani i dhahama
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Mzandiki mhaini, wala hana nia njema
Hatutaki watudhani, jinga lenye kukoroma
Jinga la moto jikoni, likizimwa hufuruma
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Huu wetu mtihani, haraka kuusukuma
Haijai kiganjani, sehemu yenye unyama
Tunakesha maofisini, bila hata kusimama
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe

Amiri msikiani, na hili ulisikize
Kibiti ni mtihani, haraka ukatatuze
Wale wana watanzani, wataka uwaliwaze
Kibiti ni fumbo gani,Amiri ulitatuwe


No comments

Powered by Blogger.