HIKI NDICHO KISA KILICHOMFANYA MWANAFUNZI KUKISHTAKI CHUO KIKUU 'UDSM' MAHAKAMANI
Mwanafunzi aliyefukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Alphonce Lusako amewasilisha maombi Mahakama Kuu aruhusiwe kukishtaki chuo hicho kwa kumkatisha masomo.
Manase
aliyekuwa akisoma shahada ya kwanza ya sheria alifukuzwa baada ya
kufutiwa usajili Januari 26, pamoja na mambo mengine akidaiwa kusajiliwa
kwa makosa kwa sababu aliwahi kufukuzwa chuoni hapo.
Lusako
anayewakilishwa na Wakili Jebra Kambole anaiomba Mahakama impe kibali
cha kuishtaki UDSM na itoe amri kuzuia uamuzi wa kumfutia usajili.
Maombi hayo yamefunguliwa chini ya hati ya dharura na yamepangwa kusikilizwa Mei 23 na Jaji Pellagia Khaday.
Hii
ni mara ya pili kwa Lusako kufukuzwa chuoni hapo, mara ya kwanza ni
Desemba 13, 2011 akiwa mwaka wa tatu akidaiwa kuchochea mgomo.
Hata
hivyo, anadai alikuwa akipinga ufisadi katika Tume ya Vyuo Vikuu (TCU)
kwa kusajili wanafunzi hewa na katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB).
Baada ya kukaa uraiani kwa muda
mrefu, aliamua kuomba usajili TCU ili kuanza upya masomo. TCU ilimsajili
na kumpanga UDSM kusoma kozi ya sheria.
Baada ya
kusoma muhula mmoja, alipewa barua ya kufutiwa usajili ikieleza
alisajili kimakosa chuoni hapo kwa kuwa tayari alishawahi kufutia
usajili.
Katika hati ya kiapo mahakamani, anadai
hakuomba usajili moja kwa moja UDSM bali aliteuliwa kihalali na TCU
yenye mamlaka ya kutathimini maombi yake na kumpangia chuo.
Anadai hakupewa haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa kanuni za haki asili kabla ya kufutiwa usajili kwa sababu zisizo halali.
Kabla ya kuwasilisha maombi mahakamani, alidai kwa mara kadhaa aliiomba UDSM imrejeshe chuoni bila mafanikio.
Lusako alijiunga na UDSM kwa mara ya kwanza mwaka 2009 akiwa amedahiliwa kusoma Shahada ya Biashara katika Uhasibu.
Mwaka
2011 pamoja na wenzake kadhaa walifukuzwa na kufutwa katika mfumo wa
elimu nchini wakidaiwa kuratibu mgomo wa wanafunzi UDSM.
Katika
mgomo huo, walikuwa wakipinga kurudishwa nyumbani wanafunzi wa mwaka wa
kwanza waliokuwa wameshawasili vyuo vikuu vya umma kwa hoja kwamba
bajeti haitoshi. Walihoji kuwapo mikopo hewa iliyokuwa ikiishia kwa
baadhi ya watendaji wasio waaminifu.
Baada ya kufukuzwa walikakata rufaa Baraza la UDSM wakiomba lirejee uamuzi wa chuo lakini baraza lilikataa maombi yao.
Agosti
30, 2012 walishinda kesi baada ya Mahakama kutupilia mbali mashtaka
dhidi yao na waliporudi chuoni, yeye na wenzake 11 waliokuwa
wameshtakiwa, lakini chuo kilikataa kuwarejesha.
source: mwananchi
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA Nini maoni yako? Weka comment yako hapa,
No comments