-->

Header Ads

WATCH: Tanzania’s Heroin Fix (Documentary)


Hivi karibuni mjadala wa matumizi na vita dhidi ya madawa ya kulevya, ulichukua sura mpya. Ingawa kwa miaka nenda rudi vita dhidi ya madawa ya kulevya imekuwepo, kila wakati imekuwa ikienda mbele na kisha kurudi nyuma. Mambo mengine huchukua kurasa za mbele. Kwa namna moja au nyingine, vita inasahaulika.

Vita iliyoanzishwa hivi karibuni ambayo kwa kiasi kikubwa ilipewa sura mpya na Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-salaam (nachelea kutaja jina kwa sababu za wazi-sijui lipi ni sahihi) imeshakumbana na changamoto zake ikiwemo kutoheshimiwa kwa misingi ya sheria na haki za binadamu.

Kadiri siku zinavyozidi kwenda, inazidi kudhihirika kwamba pengine ile vita ilikuwa ni danganya toto tu. Kuna visa na visasi nyuma ya pazia. Imekosa uhalisia na imeanza kujivika sura ya kinafiki. Waliokamatwa na waliokamata wanaelekea kuwa wanakula kutoka kwenye chungu kimoja.

Lakini wakati tukilumbana katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ni vyema kuelewa kwamba tatizo la vijana wengi kutumbukia katika dimbwi la “uteja”, linazidi kuongezeka. Vijana wanazidi kuathirika. Nguvu kazi inazidi kuteketea. Vijana wanateketea sio kwa tu kwa matumizi bali pia maambukizi ya maradhi yanayotokana na mambo kadha wa kadha mfano kuchangia sindano nk.

Swali moja ambalo nimekuwa nikijiuliza ni je; hivi tutafunga vijana wangapi? Kwanza tunayo magereza au rumande za kutosha kuwaweka vijana wote? Na kisha tukishamfunga mtu, what next? Ataacha kutumia madawa kwa kuwa tu kizuizini kwa siku kadhaa? Jibu ni kwamba ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Yatamwagika yote.

Kuna pande mbili; kwanza ni kujiuliza kwanini vijana wanaanza na kuendelea kutumia madawa ya kulevya. Majibu niliwahi kuyaandika hapa. La pili ni kupunguza athari (harm reduction). Katika mazingira ya juu juu, hili la kupunguza athari kwa kuwapa watumiaji nyenzo safi za kujidungia madawa, huonekana kama kuendekeza matumizi.

UNAWEZA KUJIFUNZA ZAIDI KUHUSU HARM REDUCTION HAPA

Hata mimi niliwahi kuwa na mtizamo huo. Lakini ukifikiria kwa undani kuhusu athari zinazotokea katika jamii mfano vifo vya vijana (kupotoea kwa nguvu kazi), maambukizi ya maradhi kama Ukimwi, na kuparang’anyika kwa jamii, utaona kwamba kupunguza athari ni jambo jema tu.

Ni vita yetu sote. Yatubidi sote tupigane. Nakukaribisha utizame documentary hii fupi ambayo inatoa picha ya jinsi vita hii inavyoweza kutafutiwa ufumbuzi

source : bongo celebrity 

No comments

Powered by Blogger.