-->

Header Ads

Waasi wa kundi la FDLR kutoka Rwanda wajisalimisha kwa UN, Congo

Idadi kadhaa ya waasi wa kundi la FDLR wa Rwanda walioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamejisalimisha kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliko mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti zinasema kuwa, waasi 15 wa kundi la FDLR wakiwemo Wacongo na Warundi kadhaa wamejisalimisha kwa askari wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika eneo la Lubero katika mkoa wa Kivu Kaskazini huko mashariki mwa Congo.

Jumuiya ya Kiraia katika eneo la Lubero imetangaza kuwa, kujisalimisha kwa waasi hao ni matokeo ya jitihada za miezi kadhaa za maafisa wa eneo hilo zinazofanyika kuwashawishi waasi wa kundi la FDLR waweke chini silaha zao na kujisalimisha wenyewe kwa askari wa Umoja wa Mataifa.

Kwa sasa waasi 66 wa kundi la Kihutu kutoka Rwanda la FDLR na wengine 291 wa makundi mengine ya waasi waliojisalimisha kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Disemba mwaka 2014, wanahifadhiwa katika kijiji cha Kanyabayonga katika eneo la Lubero.

Makundi ya waasi yanalaumiwa kuwa yamekuwa yakifanya jinai na mauaji ya kutisha katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

No comments

Powered by Blogger.