MAT wampongeza JPM kupeleka madaktari Kenya
Akizungumzia uamuzi huo, Rais wa MAT, Dk Obadia Nyongole amesema uamuzi huo utasaidia kupunguza idadi ya madaktari 1,774 waliopo nje ya mfumo wa ajira ambao wamekidhi vigezo vya taaluma.
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema uamuzi wa kupeleka madaktari nchini Kenya ambao wameombwa na Serikali ya nchi hiyo umekuja katika kipindi muafaka na unafaa kupongezwa.
Akizungumzia uamuzi huo, Rais wa MAT, Dk Obadia Nyongole amesema uamuzi huo utasaidia kupunguza idadi ya madaktari 1,774 waliopo nje ya mfumo wa ajira ambao wamekidhi vigezo vya taaluma.
Ingawa amesema uhaba uliopo nchini ni kati ya asilimia 49 mpaka 52 na kwamba kwa mikoa 13 ya pembezoni iliyoainishwa kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unafika asilimia 80, lakini hakuna jinsi kwa madaktari watakaopata ajira nje ya nchi waruhusiwe kwenda kufanya kazi.
“Madaktari wengi wapo mjini ingawa Watanzania wengi wanaishi vijijini. Hiyo inamaanisha wengi hawahudumiwi na madaktari wenye sifa. Wakati tunatoa msaada kwa majirani zetu tusisahau uhaba huu uliopo nchini,” alisema.
Amesema kwamba kwa kumbukumbu walizo nazo, mwaka jana walihitimu madktari 899 na mwaka juzi walikuwa 875.
“Madaktari wataopatikana waende kuhudumu (Kenya). Kama Serikali ya Kenya inashughulikia malalamiko ya madaktari wake, ihakikishe inaweka mazingira ya usalama kwa wageni wanaoenda kushika nafasi hizo,” amesema mtalaamu huyo wa tiba.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza daktari mmoja ahudumie watu 10,000 lakini takwimu nchini zinaonyesha uwiano huo ni kati ya wananchi 25,000 mpaka 30,000 wanaohudumiwa na daktari mmoja.
No comments