-->

Header Ads

MPYA : DUBWANA LATUTAFUNA




Himahima amkeni, twendeni kwenye mabio
Tokeni usingizini, tupunguzeni vilio
Mashariki na kusini, tuliwahini tukio
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Harahara hilo jiti, waelekezea macho
Mtumwa yake masharti, hilo wazi bila ficho
Vijana vueni shati, mzee beba pendacho
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Tukaufanye mtiti, dubwana lile uchocho
Tukavunje vizingiti, kumbe yeye kikulacho
Towashi wa tashititi,ni nini halingiacho
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Lina nyonya damu hili, latuibia pumzi
Lajionesha dhahili, pasipo na pingamizi
Suraye ya ubahili,imetupaka masizi
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Latafuna watu wengi, Huruma lisionewe
Watu wabaki vichungi, lataka linyenyekewe
Tujiwekee misingi, lenyewe likapagawe
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Acheni za Ubepari, hima tukalikabili
Tena tukiwa na ari, ili tukalidhalili
Tujipange kwa nambari,Tuwe idadi kamili
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Kulia na kwa kushoto,tazameni kotekote
Mambo mpwitompwito, asipenyeze popote
Tuliwashieni moto, lisiteme hata mate
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Dubwana hili jasiri, twendeni tukitazama
Tukiwa na tafakari, na mbinu zenye hekima
Umoja  wetu dhahiri, tupiganie kwa mema
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Twapinga usulutani,vita yetu ubwanyenye
Tuzikate hizi cheni,mapuro tuyapuziye
Haya tuzingatieni,na kazi nzuri tufanye
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili

Busara hizi pimeni,achaneni kubweteka
Niliyo nena betini, yasije yakawatoka
Jazeni na matumboni, mkapate kutosheka
Dubwana latutafuna, twendeni kulikabili
By Fulgence Makayula




1 comment:

Powered by Blogger.