-->

Header Ads

IKULU YA WHITE HOUSE YAZIDI KUKANDAMIZA WAANDISHI WA HABARI

Ikulu ya Rais wa Marekani ya White House imeyazuia mashirika kadhaa makuu ya habari nchini humo kuhudhuria kikao cha wanahabari kilichoendeshwa na msemaji wa Ikulu jana Ijumaa.


Wanahabari wa Mashirikia ya CNN, The New York Times,Politico, Los Angeles Times na BuzzFeed hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao cha wanahabari katika ofisi ya msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani Sean Spicer.
Utawala wa Rais Donald Trump umekuwa ukiyashutumu mashirika hayo kuwa yanaeneza habari za uongo na za kupotosha. Spicer hakutoa maelezo kwanini waandishi wa habari wa mashirika hayo waliachwa nje ya kikao kisicho rasmi cha wanahabari, hatua ambayo imeibua shutuma kali.
Shirika la habari la Reuters pamoja na mashirika mengine 10 yakiwemo Bloomberg na CBS yaliruhusiwa kuhudhuria mkutano huo wa wanahabari. Wakati wanahabari kutoka CNN na mashirika mengine yaliyoathiriwa yalipojaribu kuingia IKulu, yalizuiwa kwa kuambiwa majina yao hayako katika orodha ya wanahabari walioalikwa.
Trump awataja wanahabari 'adui'
Katika mkutano wa wanaharakati wa kisiasa wa jumuiya ya wahafidhina ya CPAC hapo jana, Ijumaa, Rais Trump alivishutumu baadhi ya vyombo vya habari ambavyo anadai vinatoa taarifa za uongo na kuvitaja kuwa adui ya watu wa Marekani.
Spicer amesema kundi lake liliamua kufanya mkutano mdogo wa wanahabari katika ofisi yake badala ya mkutano rasmi wa wanahabari kama ilivyo desturi katika chumba cha wanahabari katika Ikulu ya Rais akihoji hawahitaji kuendesha kila kitu mbele ya kamera kila siku.
Wanahabari kutoka mashirika ya Associated Press na Jarida la Time waliondoka kutoka kwenye kikao hicho walipoarifiwa kuwa wanahabari wenzao kutoka mashirika mengine wamezuiwa kuhudhuria kikao hicho.
Taarifa kutoka kwa mhariri mkuu wa The New York Times Dean Baquet imesema jambo kama hilo halijawahi kutokea katika Ikulu ya Rais ya White House katika historia yao ndefu ya kuripoti taarifa kutoka tawala chungu nzima kutoka vyama tofauti vya kisiasa nchini Marekani.
Baquet amesema wanapinga vikali kuzuiwa kwa gazeti lao na mashirika mengine ya habari na kuongeza kuruhusiwa kwa vyombo hivyo kuwa na uhuru na kuangazia matukio ya serikali iliyo wazi bila shaka ni muhimu kwa maslahi ya taifa.
Chama cha maripota wa Ikulu ya White House WHCA pia kimepinga hatua hiyo ya Spicer. Rais wa chama hicho Jeff Mason ambaye ni ripota wa Reuters amesema wanapinga vikali jinsi kikao cha Ijumaa kilivyoendeshwa na Ikulu ya White House.
Uhusiano kati ya Trump na wanahabari si mzuri
Katika kipindi cha kampeini mwaka jana, kundi la Trump liliyapiga marufuku mashirika kadhaa likiwemo gazeti la Washington Post na Buzzfeed dhidi ya kuripoti katika mikutano ya kampeini likiyashutumu kwa upotoshaji ba kueneza habari za uongo.
CNN iliandika katika ukurasa wake wa Twiiter ikisema kitendo cha kuzuiwa kwa baadhi ya mashirika ya habari sio jambo linalokubalika kutoka kwa utawala wa Trump na huenda ndivyo Ikulu ya Rais inavyojiendesha wakati taarifa za kweli ambazo hawazipendi zinaporipotiwa.
CNN imeapa kuendelea kuripoti licha ya hatua kandamizi kama hizo. Mhariri mkuu wa BuzzFeed Ben Smith pia ameishutumu Ikulu ya rais Donald Trump kwa kuyaadhibu mashirika ambayo yanaangazia taarifa ambazo hawapendi ziangaziwe na kuendelea kusema hawatasita kuripoti kuhusu utawala huo mpya wa Marekani kwa njia iliyo huru na ya haki.
Spicer amesema Ikulu ya Marekani inapanga kupambana dhidi ya kile alichokitaja kuangaziwa kionevu na vyombo vya habari. Msemaji huyo wa Ikulu ameeleza kuwa hawatakaa tu na kuruhusu taaarifa za uongo na za kupotosha zikitolewa.
SOURCE : DW

No comments

Powered by Blogger.