-->

Header Ads

UVCCM: Huu si wakati wa kuabudu cheo cha Mtu


Mwenyekiti wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheir James, amesema wakati wa kufanya kazi kwa woga ndani ya umoja huo umepitwa na wakati.

Akizungumza na wanachama wa CCM na jumuiya zake visiwani Zanzibar, alisema huu ni wakati wa kufanya kazi kwa ushirikiano badala ya kumuabudu mtu kutokana na cheo chake.

Alisema kiongozi anayejitambua ni yule anayefanya kazi kwa maslahi ya vijana wenzake na kilichobaki kwa sasa ni kupambana ili jumuiya hiyo ya vijana iweze kufika mbali kwa maslahi ya vijana na taifa kwa ujumla.

Aidha, alisema wakati wa vijana wanaopenda kulalamika umefika mwisho hivyo ni vyema wakajitahidi kufanya kazi bila ya upendeleo na woga.

Aliwataka viongozi wenzake katika jumuiya hiyo kuanza kuhakiki mali za chama na aliyekuwa haendani na kasi ya chama hicho awapishe wanaoweza.

"Umegombania nafasi na tumekupa, sasa tufanyeni kazi ili vijana wajue thamani ya uongozi," alisema.

Kheir alisema uhakiki wa mali za chama hicho kwa upande wa Zanzibar utafanywa na Wazanzibari wenyewe na atahakikisha anapatiwa ripoti ya uhakika kwenye taarifa watakazozipeleka kwa uongozi wa juu na uhakiki wa watumishi hewa pia utaangaliwa.

Makamo Mwenyekiti wa Umoja huo, Tabia Maulid Mwita, alisema yupo tayari kufanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu na vijana wote na kuwashukuru kwa kumchagua kushika nafasi hiyo na kuendeleza ahadi zake alizoziahidi kipindi cha kampeni.

Aidha, aliwataka vijana kuacha makundi kwa kuwa uchaguzi umekwisha hivyo atahakikisha haki inatendeka bila ya kumuonea mtu wala kujali cheo chake na kufanya maamuzi kwa matakwa yake bila ya kumshauri mtu.

"Vijana ndio jeuri ya chama ila kwa anayejitambua na sio kukaa kutukana katika majukwaa kijana mzuri ni yule anayependa kusikiliza ushauri wa wakubwa wake," alisema.

Mapema akitoa utambulisho kwa viongozi, Kaimu Katibu wa Umoja huo Zanzibar, Abdulghafar Idirissa Juma, alisema Umoja huo utaangalia upya vitega uchumi vyake ili viweze kuleta tija kwa wanachama na kuiendeleza jumuiya yao.

Akizungumzia mradi wa Darajani alisema kuwa ulihodhiwa na baadhi ya viongozi wa serikali hivyo alimtaka Mwenyekiti wa Umoja huo kulifuatilia suala hilo ili mipango iendelee na mradi huo uweze kuleta tija kwa vijana na taifa kwa ujumla.

No comments

Powered by Blogger.