Mbonde amrithi Banda Simba SC
SALIM MBONDE.
SIKU mbili tu baada ya Abdi Banda kusaini rasmi mkataba wa miaka mitatu wa kuitumikia klabu ya Baroka FC ya Afrika Kusini, klabu ya Simba haraka jana ilimsainisha mkataba wa miaka miwili beki wa Mtibwa Sugar na timu ya Taifa 'Taifa Stars', Salim Mbonde.
Mbonde amesaini mkataba huo saa chache baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitokea Afrika Kusini alipokuwa na kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki michuano ya Cosafa.
Taarifa ya klabu ya Simba imeeleza beki huyo alisaini mkataba huo mbele ya mfadhili na mdau mkubwa kwa klabu hiyo mfanyabiashara, Mohamed Dewji maarufu kwa jina la Mo.
"Sasa ni rasmi Mbonde, ni mchezaji wa Simba baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, tunaamini atakuwa msaada mkubwa kwa timu yetu," ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Kwa upande wake, Mbonde aliliambia Nipashe kuwa amefurahi kusaini kwenye timu hiyo na anaamini huo ni mwanzo mzuri kwake kusonga mbele zaidi.
Mbonde alikuwa 'pacha' wa Banda kwenye kikosi cha Stars kilichoshiriki Cosafa ambapo waliisaidia timu hiyo kushika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo iliyomalizika jana.
Banda, ambaye alisajiliwa na Simba akitokea Coastal Union, mkataba wake ndani ya klabu hiyo umemalizika na licha ya uongozi wa Simba kutaka kumuongezea mwingine ameamua kusaini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo ya Afrika Kusini.
No comments