ALICHOSEMA AVEVA JUU YA MALALAMIKO YA YANGA
WAKATI Yanga wakilia na Bodi ya Ligi kuipa Simba pointi tatu za Kagera Sugar, Rais wa Wekundu hao Evans Aveva amesema kuwa Kamati ya Masaa 72 imefanya kazi kwa uaminifu mkubwa hivyo Yanga waache kupiga kelele kwani hazitawasaidia.
Kamati hiyo ilitoa uamuzi huo juzi Alhamisi kwamba beki wa Kagera Sugar, Mohamed Fakih alicheza mechi yao akiwa na kadi tatu za njano ambapo Simba waliwasilisha malalamiko yao ili kamati itoe ufafanuzi na kuchukuwa hatua. Mechi hiyo Simba ilifungwa bao 2-1.
Aveva alisema kuwa wanashukuru kamati kutoa pointi hizo ambazo walikuwa na uhakika nazo hivyo sasa wapo katika mapambano ya kuhakikisha hawafanyi makosa kwenye mechi zao zilizobaki ambapo leo Jumamosi wanacheza na Toto Africans uwanja wa CCM Kirumba.
“Tumewasikia wenzetu wanavyolalamika na kutaka kwenda mahakamani lakini unakimbiliaje mahakamani kukata rufaa wakati kuna kamati zingine za michezo za kukata rufaa, wakishindwa huku ndipo waende mahakamani.
“Kamati hii imetoa maamuzi sahihi na wametenda haki kwani tulipeleka malalamiko ambayo wameyafanyia kazi na haki yetu tumepata, isingekuwa kweli basi hii haki tusingepata na ingekuwa aibu yetu,” alisema Aveva.
Baada ya kupewa pointi hizo Simba sasa wamefikisha pointi 61 na kuwaacha Yanga wakiwa na pointi 56.
No comments