-->

Header Ads

AKUPENDE NANI














Unajipa kazi nyingi, kuvimaliza viunga
Mume asikate ringi, na sindino wajidunga
Hujui lipi la msingi,umekuwa kama nanga
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani

Washinda mitandaoni, kutafuta viongeza
Ufutuke tu nyumani, ubane vya kulegeza
Huna amani moyoni, akili unabobeza
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


Walikuwako zamani, mababu na mabibizo
Mafundi wa kitandani, wa mababu kitulizo
Walichoongeza nini, kuutafuta ujazo
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


Unahangaika nini, mpaka unapauka
Kutuvalia kimini, huoni unaumbuka
Tamu ya penzi amani, ijenge itajengeka
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


Ongezea na hekima, ipate kuimarika
Uzingatie heshima, pasipo kujali rika
Busara iwe kisima,na iweze kuchoteka
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


Mume kama dunia, haidhiriki kwa umbo
Acha kuhangaikia, utapoteza urembo
Utakuja kujutia, utapobakia fimbo
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


Unaongeza midomo, unaongeza matako
Unajichimbia shimo, mume umpe makoko
Utarefusha na kimo, na kubadili misuko
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


Unaongeza matiti, unabadilisha rangi
Unajenga vizingiti, wamkosa bwana mangi
Huna mvuto thabiti, ni kweli ya Mungu mengi
Usijisumbue dada, na utapendwa na nani


No comments

Powered by Blogger.