-->

Header Ads

MAAJABU YAWAGOMEA BARCELONA

MAAJABU yamekataa! FC Barcelona imeshindwa kupindua matokeo ya mabao 3-0 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus baada ya jana kulazimishwa sare ya bila kufungana kwenye uwanja wa Nou Camp.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Juventus Arena miamba hiyo ilipoteza mchezo huo kwa mabao hayo hivyo suluhu ya jana ikawa tiketi ya kutupwa nje ya michuano.

Katika mchezo wa hatua ya 16 bora Barcelona ilifanya maajabu ya kutoka nyuma kwa mabao 4-0 dhidi ya PSG ya Ufaransa kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kabla ya kushinda mabao 6-1 kwenye uwanja wa Camp Nou na kufika hatua ya robo fainali ambapo imehitimishwa na Juve.

Vijana wa kocha Massimiliano Alegri walicheza kwa nidhamu kubwa hasa safu ya ulinzi ambayo iliweza kuwadhibiti washambuliaji wa Barcelona Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar waliokuwa wakihaha kusawazisha mabao hayo.

Mchezo mwingine AS Monaco nayo imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga Borussia Dortmund mabao 3-1 na kuwatoa kwa jumla ya mabao 6-3 kufuatia ushindi wa 3-2 walioupata kwenye uwanja wa Signal Iduna Park wiki iliyopita.

Mabao ya Monaco yalifungwa na Kylian Mbappe dakika ya tatu, Radamel Falcao (17) na Valere Germain dakika ya 81 huku Marco Reus akiwafungia Dortmund bao la kufutia machozi.

Monaco na Juve zinaungana na Real na Atletico Madrid katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo droo yake itafanyika kesho Ijumaa.

No comments

Powered by Blogger.