HUU NDIO UGONJWA MBAYA TANZANIA Dalili ni Kutoka Damu Mfululizo ..Matibabu Yake ni Milioni 200 kwa Mtu Mmoja.SOMA HAPA KUUFAHAMU
TAKRIBANI Watanzania 5,400 wanaugua ugonjwa wa himofilia, huku wataalamu
wakibainisha kuwa wanaojulikana na kupatiwa matibabu katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) ni 100 pekee.
Himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda pale mtu anapopata
jeraha, kwa kukosa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini
zinazotakiwa kugandisha damu na kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu.
Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu wa MNH, Dk. Stella Rwezaura,
aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu ugonjwa huo uliogundulika mwaka 2009.
Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania 10,000,
mmoja anaugua ugonjwa huo ambao kwa asilimia 70 unatokana na kurithi
kutoka kwenye vinasaba vya kike na asilimia 30 kwa mabadiliko ya
vinasaba.
“Watanzania wengi hupeleka watoto wao kwenda jando bila kuwapima kama
wana ugonjwa wa himofilia au la, na wapo wanaopoteza maisha kwa sababu
hiyo, ni muhimu kuwapima hata kabla ya upasuaji,” alisema.
Alisema kwa sasa kuna madaktari bigwa wa damu 10 pekee nchini huku
wahudumu wa afya wengi wakiwa hawana uelewa wa ugonjwa huo tishio.
Kwa mujibu wa Rwezaura tiba ya ugonjwa huo huanza kutolewa tangu mtoto
anapokuwa na umri wa miaka mitatu na hufundishwa kujichoma sindano
maalumu za dawa hizo anapofikisha umri wa miaka nane. Dk.
Rwezaura alisema kuna aina tatu za himofilia ambazo ni pamoja na
himofilia A inayowapata wengi kwa kukosa chembechembe za kugandisha
damu.
Nyingine ni himofilia B ambayo huwapata wagonjwa wachache wenye upungufu
wa chembechembe namba tisa na wenye himofilia A na B ambayo mgonjwa
huvuja damu kwa muda mrefu kuliko kawaida.
Alibainisha kuwa mgonjwa anaweza kupoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi
bila matibabu kwa kuwa hakuna chembechembe za kuzuia damu kutoka na
kwamba viunganishi vya mwili, mfano magoti, kiwiko na uti wa mgongo
wakati mwingine huvimba kutokana na damu kuvujia ndani na baadaye
kusababisha ulemavu. Dk. Rwezaura alisema himofilia mbaya zaidi ni ile
ambayo damu huvujia kwenye ubongo kwa kuwa ni nadra mgonjwa kupona.
"Hadi sasa, hospitali inayotibu ugonjwa huo ni Muhimbili tu. KCMC na Bugando wanatoa vipimo vya awali," alisema.
Awali akisoma hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, juu ya ufunguzi wa mkutano huo,
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Prof. Ayoub Magimba,
alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2008,
zinaonyesha kuwa takribani vifo milioni 36 duniani vilitokana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwamo ugonjwa huo.
“Kulingana na takwimu za Shirika la Himofilia Duniani (WHF), watu
400,000 wanaishi na himofilia duniani. Kati yao, asilimia 25 ndiyo
wanaopata matibabu,” alifafanua Prof. Magimba.
Katika hotuba hiyo, Waziri Ummy alisema serikali inatambua kuwa ugonjwa
huo ni mkongwe kama maeneo mengine duniani, lakini jamii haina ufahamu
wa kutosha na kwamba wengi wa wataalamu wa tiba nao hawana ufahamu wa
kutosha pia.
Waziri huyo alisema inakadiriwa kuwa asilimia 97 ya watu wenye himofilia
hawajui kama wanao na hawajawahi kupima na kwamba utafiti umebainisha
kuwa hatua madhubuti zikichukuliwa, mgonjwa ataweza kuishi maisha ya
kawaida bila kuathiri mwili na kuepuka kupata ulemavu.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili jamii ya watu wenye
himofilia ni uelewa mdogo, dawa na vipimo tiba, wataalamu wa tiba
kutokuwa na uelewa wa kutosha, waganga wa tiba asili na ghariba kufanya
tohara bila tahadhari.
Waziri huyo alizitaja changamoto nyingine kuwa ni wazazi na wagonjwa
kukosa uelewa na ukosefu wa vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa zaidi
ya Muhimbili.
“Tanzania imedhamiria kushirikiana na wadau wa himofilia katika
kufikisha elimu ya uenezi katika jamii nzima. Serikali itaendelea na
utekelezaji wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambayo iko kwenye hatua za
mwisho za marekebisho,” alifafanua zaidi Ummy katika hotuba hiyo.
Rais wa Chama cha Himofilia Tanzania, Richard Minja alisema madhara
yaliyojitokeza katika familia ni wanaume kuzikimbia familia zao baada ya
watoto kubainika kuwa na ugonjwa huo.
Alisema ni lazima kuwe na utekelezaji wa kauli mbiu ya mwaka huu ambayo
ni 'uvujaji damu, ulemavu na vifo vitokanavyo na himofilia sasa basi'.
Minja alisema kwa sasa dawa za ugonjwa huo zinatolewa kwa msaada na watu
wa Marekani na kwamba mgonjwa kupata dawa za mwaka mzima anatakiwa kuwa
na dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh. milioni 200), lakini kwa sasa
matibabu yanatolewa bure nchini.
“Mgonjwa anatakiwa kuongezewa chembechembe mara mbili kwa wiki, pia
inashauriwa awe nazo muda wote nyumbani ili inapotokea ameumia anatumia.
Pia wanatakiwa kufanya mazoezi na kuepuka kuumia,” alisema.
Aliitaja tiba nyingine ya ugonjwa huo kuwa ni 'plasma' inayotokana na
chembechembe za damu ya watu wengine ambapo wataalamu huchuja
chembechembe hizo kutoka kwenye benki za damu.
Alisema katika kliniki ya Muhimbili kuna wastani wa wagonjwa watano hadi
10 kwa wiki wanaoendelea na matibabu. “Damu ikivuja kwa muda mrefu bila
matibabu husababisha madhara makubwa na hata kifo, kwani huathiri
magoti, mifupa ya fahamu na kusababisha ulemavu.
Kifo hutokea iwapo damu itavuja kwa muda mrefu kwenye viungo muhimu kama ubongo, uti wa mgongo na tumbo bila kutibiwa," alisema.
Minja alisema kuna dawa maalumu za sindano za ugonjwa huo na wagonjwa
hawapaswi kumeza dawa za kutuliza maumivu isipokuwa panadol.
Abdulsaid Mgima, mgonjwa wa himofilia, alisema aligundulika kuwa na
ugonjwa huo akiwa na umri wa miaka 10 akiwa mkoani Mbeya baada ya wazazi
wake kuhangaika kumtibu bila mafanikio hadi alipopelekwa Muhimbili.
"Ugonjwa ulianzia kwenye mkono (umepinda), lakini naendelea na shughuli
zangu.
Ninaiomba serikali itambue ugonjwa huu na kuwafikia watu wengi zaidi
hususani vijijini," alisema. Cecilia Swai alisema kuwa alipoteza mtoto
mwaka 2013 kutokana na ugonjwa huo baada ya kukosa dawa za ugonjwa huo.
Alisema mtoto wake aliugua kwa siku tatu na alipofikishwa Muhimbili,
hakukuwa na dawa za kumsaidia hivyo akafariki dunia. Kwa mujibu wa Dk.
Rwezaura, wagonjwa sita walipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu
Muhimbili kabla hospitali hiyo haijapata dawa ya kutibu ugonjwa huo.
JIUNGE NASI AKISI TV KILA SIKU KUPATA HABARI ZA UHAKIKA
Nini maoni yako? Weka comment yako hapa
No comments